Habari MsetoSiasa

Kuria na Kimani Ngunjiri wazidi kupondwa

January 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na FRANCIS MUREITHI

SHIRIKA moja pamoja na usimamizi wa chama cha ODM kaunti ya Nakuru vimekashifu matamshi ya wabunge Kimani Ngunjiri wa Bahati na Moses Kuria wa Gatundu Kusini, wakisema walidunisha afisi ya Rais.

Mwenyekiti wa shirika hilo Jesse Karanja alisema kuwa matamshi ya wabunge hao ni hatari kwani yanachochea uhasama wa kijamii nchini, wakati Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanapambana kuunganisha taifa.

“Matamshi yao yasiyofaa yanahatarisha kuleta woga, kuchanganyikiwa na utengano miongoni mwa jamii tofauti na wafuasi wa mirengo ya kisiasa nchini,” akasema Bw Karanja.

Katibu wa ODM Nakuru Hilton Abiola alizitaka mamlaka za serikali zinazohusika kuchunguza matamshi ya viongozi hao.

“Tunataka Bw Ngunjiri achukuliwe hatua za mara moja kwani ameonyesha chuki dhidi ya baadhi ya jamii kama alivyojaribu kumtimua Bw Odinga Nakuru mnamo 2016,” akasema Bw Abiola.

Bw Karanja alisema kuwa matamshi ya viongozi hao hayawakilishi yale ya wafuasi wa Jubilee kutoka eneo la Mlima Kenya na kaunti ya Nakuru.

“Hawa ni viongozi wa kibinafsi na wanaokuza ukabila, wanafaa kumheshimu Rais kwani ndiye ishara ya umoja wa kitaifa na udhabiti na hivyo anastahili heshima kutoka kwa wanasiasa wote,” Bw Karanja akasema.

Viongozi wengine ambao wamekashifu matamshi ya Bw Ngunjiri ni mshirikishi wa baraza la wazee wa jamii ya Kalenjin Andrew Yatich na Bw Chris Wathimba ambaye ni mwenyekiti wa wawaniaji wa eneobunge la Bahati.