Kuwajali wakulima wa mahindi na miwa ni kukosa busara – Moses Kuria
Na PETER MBURU
MBUNGE wa Gatundu Kusini ameibua ghadhabu miongoni mwa Wakenya, baada ya kutoa pendekezo tatanishi kuwa hakuna haja ya kuwajali wakulima wa mahindi na miwa tena, na badala yake bidhaa hizo zitafutwe kutoka mataifa jirani.
Kupitia akaunti yake ya Facebook Jumanne, Bw Kuria alisema badala ya kununua sukari na mahindi kutoka kwa wakulima wa humu nchini, ambazo ni ghali, ni vyema kununua bidhaa hizo kutoka Uganda.
Alitaja suala la kununua bidhaa za Wakenya kuwa “kulinda sekta zisizojiweza”, akitaja hali hiyo kuwa “isiyowezekana wala isiyo ya busara.”
“Napendekeza kuwa tufungue mpaka wetu na Uganda kikamilifu ili sukari na mahindi yanayotolewa humo yachukuliwe asilimia 100 kama yaliyotolewa Kenya. Hii inafaa kuendelea hadi tuweze kutengeneza sukari na mahindi kwa bei ambazo zinawiana na Uganda,” Bw Kuria akasema.
“Maslahi ya watumizi wa bidhaa yanafaa kuwekwa mbele ya yale ya wakulima. Aidha tulainishe ama tukimye. Kulinda sekta zisizoweza kwa karne haiwezekani wala haina busara.”
Hata hivyo, matamshi ya Bw Kuria yalikumbana na ghadhabu ya Wakenya na pingamizi kali, huku pia kiongozi mwenzake katika hafla tofauti akikosoa suala la kuwezesha wananchi wa mataifa jirani wakati wa humu nchini wanaangamia.
Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Baringo, Bi Gladwell Cheruiyot alikashifu kuidhinidhwa kwa wafanyabiashara kuleta bidhaa kutoka mataifa jirani kushindana na za Wakenya humu nchini, wakati gharama ya kuzitengeneza si sawa.
“Ufisadi umeua sekta ya chakula humu nchini na sasa tumeanza kuwavunja moyo wakulima na ukuzaji wa vyakula,” Bi Cheruiyot akasema, japo hakuwa akimjibu Bw Kuria.
Lakini Wakenya ambao haswa walikerwa na pendekezo la Bw Kuria walimkumbusha kuwa hali ya bidhaa humu nchini kuwa ghali imesababishwa na ulipaji kodi ya juu, jambo ambalo si sawa katika mataifa jirani.
Wengi wa Wakenya aidha walimkemea mbunge huyo kwa kupendekeza kunyanyaswa kwa wakulima wa miwa na mahindi, ilhali hivi majuzi alikuwa akiwatetea wale wa kahawa.
“Ni serikali ambayo imetoza ushuru dawa za kunyunyizia mimea na kupandisha ushuru wa VAT hivyo kufanya mchakato wa kukuza vyakula hivyo kuwa ghali na mwishowe bidhaa ya mwisho kuwa ghali sana na kuwafaidi wakulima wakubwa pekee,” Musa Wa Kibui akasema.
Wakulima zaidi walielezea kuhusu matatizo wanayopitia kukuza mimea hiyo, ilhali mwishowe hawavuni matunda yoyote.