Habari Mseto

LADY HEKMA: Mpango mzima ni kumpiku Lupita Nyong'o kwa uigizaji

February 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

‘Mtaka cha mvunguni sharti ainame.’ Ndivyo wahenga walivyologa na tangia zama zile ndivyo hali ilivyo hadi sasa. Ni msemo ambao umeonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii.

Pia msemo huo unaonekana unaendelea kudhihirishwa na vijana wengi tu ambao hujituma kuchapa vibarua bila kulegeza kamba kwenye jitihada zao kusaka jinsi ya kujikimu kimaisha.

Kati yao ni dada huyu mwenye umbo la kuvutia ambaye licha ya mwanzo kuwa mwanamuziki wa densi baadaye amejikuta akijihusisha na talanta kadhaa ikiamo maigizo.

Dah! Unajua imekuaje? Dada huyo anasema katika maigizo ameazimia hata kumpiku mwigizaji anayetamba katika filamu za Hollywood, Mkenya Lupita Nyong’o.

Je ni nani huyu? Dah! Usikonde, siyo mwingine bali, Rosemary Wairimu Githu anayefahamika kama Lady Hekma kwa jina la msimbo.

Katika mpango mzima, Lady Hekma mzawa wa eneo la Magongo mjini Mombasa ambaye amejaliwa watoto wawili ni mwanamuziki/rapa, mwinjilisti, mwandishi wa filamu na mistari ya nyimbo za injili, mwigizaji, prodyuza wa filamu pia anatajriba ya utangazaji.

Kwenye uinjilisti ndiye mwanzilishi wa kanisa la Selah Restoration Ministry International. Katika utangazaji huandaa shoo ya Eden Gospel pia Hip/Hop Creative Thursday kwenye mtandao wa jamii wa Facebook.

Rosemary Wairimu Githu. Picha/ John Kimwere

”Bila shaka siyo rahisi kutia kapuni talanta zote hizi wala siyo kwa nguvu zangu mwenyewe bali yote ni kwa neema yake Mwenyezi Mungu Muumba,” anasema na kuongeza hakuna lisilowezekana kwa uwepo wake.

Lady Hekma akishirikiana na mumewe, Kennedy M. Nyamai wanamiliki kampuni ya Edenpix Media ambayo ina vitengo kadhaa ikiwamo Music Factory Beats na Edenpix Films.

Lady Hekma anasema kama prodyuza amefaulu kuzalisha muvi iitwayo ‘Dark Prayer,’. ”Sijashiriki kwenye filamu hiyo kama mwigizaji bali mimi ndiye prodyuza,” alisema na kuongeza kwamba katika kitengo hicho ameazimia kufikia upeo wake Alison Ngubuini aliyehusika pakubwa kutayarisha baadhi ya muvi zilizowahi vumisha sekta ya maigizo nchini kama Mali, Sugar na Siri kati ya zingine.

Aidha amekusudia kuanzisha kipindi kiitwacho ‘Grace Show’ kinachonuiwa kurushwa kwenye mojawapo kati ya televisheni za humu nchini. Pia anajiandaa kuachia albamu ya tambo za injili inayotarajiwa kujumuisha fataki kama ‘Hakuna Mungu kama wewe,’ ‘Wewe ni Mwema,” ‘Back to basics,’ ‘New Creation,’ ‘Kazi kamilifu,” na ‘Alinipenda,’ kati ya zingine.

Katika maigizo, Lady Hekma alifanikiwa kutoa muvi ya kwanza mwaka 2009 iliyokwenda kwa jina ‘Kinaya’ lakini haikubahatika kuonyeshwa popote. Tangia arejelee masuala ya filamu miaka mitatu iliyopita, ametoa muvi mbili, ‘Dalifa’, na ‘Zandiki,’ zilizofaulu kurushwa kwenye runinga ya K24 mwaka jana na mwaka huu kupitia kipindi cha Kenya Film Night.

Kwenye kazi ya muvi ya Dalifa kando na kuwa mwandishi pia alihusika kama prodyuza na kuigiza akiwa rafiki wa mhusika mkuu aliposhiriki nafasi ya mrembo Lolita.

”Ningependa kufafanua kuwa katika uinjilisti mimi hutoa huduma za injili ya Bwana wala sihitaji sadaka yoyote naelewa watu wengi huenda wakaanza kudai mimi mwenye tamaa ya fedha,” alisema na kuongeza kuwa utunzi wa nyimbo na maigizo ndiyo tegemeo lake ikiwa ni ajira kama nyinginezo.

Nawahimiza waigizaji wanaokuja kutovunjika moyo bali wajitume kwa kujitolea bila kulegeza uzi maana bidii yao ndiyo itawafanikisha kufunguka kwa milango. Pia anawashauri kuzingatia suala la kuandikiana mkataba ili kujiepusha dhidi ya waajiri ambao hupenda kutumia jasho la wasanii chipukizi kujifaidi.