• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:50 AM
LAPSSET: Serikali yakana madai ya kubagua vijana katika ajira

LAPSSET: Serikali yakana madai ya kubagua vijana katika ajira

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kitaifa imekanusha madai kwamba vijana wa Lamu wanabaguliwa katika ajira kwenye ujenzi unaoendelea wa Bandari ya Lamu (LAPSSET).

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu serikali Sh2.5 trilioni unaendelezwa eneo la Kililana.

Tayari asilimia 60 ya ujenzi wa viegesho vitatu vya kwanza vya LAPSSET umetekelezwa huku kiegesho cha kwanza kikitarajiwa kukamilika kufikia mwishoni mwa Juni mwaka huu.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Jumapili, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, alisema msimamo wa serikali ni kuhakikisha miradi inayoendelezwa na serikali kuu kaunti ya Lamu inafaidisha wakazi wa eneo hilo moja kwa moja.

Bw Kanyiri hata hivyo alitamaushwa na ripoti ya hivi majuzi kutoka kwa Wizara ya Ujenzi na Nyumba, iliyofichua kuwa ni vijana 50 pekee kutoka Lamu kati ya 1,200 wanaofanya kazi katika LAPSSET.

Bw Kanyiri alisema idadi hiyo ndogo haitokani na ubaguzi unaodaiwa na baadhi ya wakazi dhidi ya vijana wa Lamu.

Badala yake, alisema baadhi ya vijana wa Lamu wamekuwa wakibagua kazi na pia kufanya kazi kwa muda tu na kisha kuacha kazi hizo punde wanapoajiriwa.

Aliwashauri vijana kutobagua kazi hasa zile zilizoko kwenye miradi ya serikali ya kitaifa, ikiwemo LAPSSET na ujenzi wa barabara ya Lamu hadi Garsen.

Alisema serikali itahakikisha vijana wa Lamu wanapewa kipaumbele katika ajira kwenye miradi hiyo, hivyo kuwahimiza kufika maeneo ya miradi ili waajiriwe.

Alisema baadhi ya vijana husubiri hadi matangazo ya kazi yatolewe.

Alisema ni vyema kutafuta kazi hizo wao binafsi hata kabla hazijatangazwa.

“Serikali haina nia ya kubagua kijana wa Lamu kwa misingi yoyote ile, iwe ni dini, kabila au eneo mtu anatoka. Cha msingi ni hao vijana wawajibike ipasavyo kwa kufika kwenye maeneo ya miradi na kuulizia kazi hizo.”

Kuna baadhi ya vijana wamekuwa wakibagua kazi. Wengine wanadai malipo ni ya chini ilhali wengine wakisema kazi ni ngumu. Hakuna kazi rahisi. Jitolee ufanye kazi yoyote ilmradi upate fedha za kukimu maisha yako. Cha msingi ni wewe kuitafuta kazi hiyo kwani haitakufuata mlangoni,” akasema Bw Kanyiri.

Kauli ya kamishna huyo inajiri siku chache baada ya wakazi wa Lamu wakiongozwa na wanachama wa baraza la wazee, akina mama na vijana kujitokeza kuikashifu serikali kwa kuwabagua wakazi wa Lamu kiajira hasa katika LAPSSET.

Wakazi hao pia waliitaka serikali kuomba msamaha kwa kauli yake ya hivi majyuzi kwamba wakazi ni wavivu katika kufanya kazi kwenye eneo la bandari ya Lamu (LAPSSET).

You can share this post!

Wapokomo na Waorma kuungana kisiasa

Nyoka wavamia pasta akitimua mapepo

adminleo