Habari MsetoSiasa

Lazima nishirikiane na upinzani – Ruto

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

VALENTINE OBARA na DENNIS LUBANGA

NAIBU Rais William Ruto, ameapa kuendelea kushirikisha viongozi wa mirengo tofauti ya kisiasa katika ziara zake kitaifa.

Huku akitetea ziara hizo na kusema ni za maendeleo, Bw Ruto alisema ushirikiano huo ni muhimu kuleta mabadiliko kwa maisha ya Wakenya.

“Inatia moyo jinsi viongozi wote waliochaguliwa wameamua kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya Wakenya. Ni kweli kwamba umoja pekee ndio unaoweza kufanikisha maendeleo,” akasema akiwa Bungoma jana.

Matamshi hayo yalitokea wakati ambapo Chama cha ODM kimeeleza nia ya kuwatimua wabunge Aisha Jumwa (Malindi) na Suleiman Dori (Msambweni) kwa kwenda kinyume na sera za chama walipoandamana na Bw Ruto katika ziara zake Pwani na kuonekana kuunga mkono azimio lake la urais ifikapo mwaka wa 2022.

Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Christ the King Cathedral, Bw Ruto alipuuzilia mbali viongozi wanaohusisha kila hatua anyaochukua na siasa za 2022 akataka wakome kuzungumzia siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta na badala yake watumikie Wakenya kikamilifu.

“Wakati wa siasa haujafika. Huu ni wakati wa kutilia maanani miradi ya maendeleo ambayo yanahusu maisha ya wananchi wetu moja kwa moja. Bado tuna wakati hadi 2022 kuleta umoja na kutumikia wananchi,” akasema.

Alikuwa ameandamana na Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati, wabunge Enock Kibunguchi (Likuyani), Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), John Waluke (Sirisia), James Lusweti (Kabuchai), Didmus Baraza (Kimilili) na Moses Mabonga (Bumula).

Bw Wangamati alisema wako tayari kumuunga mkono Bw Ruto akiwania urais 2022 kwani jamii ya eneo la Magharibi linataka kuwa serikalini.

“Watu wetu hawawezi kukaa katika upinzani kwa zaidi ya miaka 15. Tuko tayari kuungana na upande wa ushindi ndiposa tutakuunga mkono kikamilifu wakati huo ukifika,” akasema.

Viongozi wengine waliozungumza pia waliunga mkono azimio la naibu rais kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.