Lazima ushtakiwe kwa kumdhalilisha Rais, mahakama yamgomea Waititu
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amepata pigo kuu baada ya mahakama kukataa kufitilia mbali kesi ya kumdhalalisha Rais William Ruto Septemba 29, 2024.
Akikataa kuharamisha kesi aliyoshtakiwa Bw Waititu, hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina alisema shtaka alilofunguliwa mwanasiasa huyo halina dosari kisheria.
“Shtaka alililoshtakiwa Bw Waititu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) halina dosari na naamuru alijibu,” Bw Onyina aliamuru.
Gavana huyo wa zamani alikana alimdhalilisha Rais Ruto kwa kutumia lugha chafu iliyokusudiwa kuvuruga amani.
Hakimu alisema shtaka dhidi ya Bw Waititu linaambatana na vipengee vyote vya na kwamba “anatakiwa kujibu shtaka na kesi kuendelea hadi tamati.”
Mbunge huyo wa zamani wa Embakasi alikana shtaka la kumtusi Rais Ruto alipohutubia umati wa watu katika uwanja wa Ruiru kaunti ya Kiambu.
“Shtaka dhidi ya Waititu linambaatana na Kifungu nambari 334 na 137 za sharia za uhalifu. Iikiwa nitaitupilia mbali basi nitakuwa nimetumia vibaya mamlaka niliyopewa na sheria vibaya,” alisema Bw Onyina.
Hakimu alitupilia mbali ombi la Bw Waititu la kuharamishwa kwa kesi dhidi yake aliyowasilisha kupitia mawakili wake Martha Karua, Levi Munyeri na Ndegwa Njiru akidai linakinzanana na sharia.
Mawakili walisema kesi hiyo inakiuka haki za mshtakiwa kwa vile “maneno anayodaiwa alimdhalilisha Rais Ruto ni maoni yake kuhusu hali ilivyo nchini.”
Bw Waititu alishtakiwa kudai wakenya walidanganywa kwamba mambo yatakuwa shwari nyakati za kampeini lakini maisha yamekuwa magumu.
Waititu alishangaa ni jinsi gani alimshushia hadhi Rais Ruto kwa kudai mama mboga na mahasla walidanganywa kisha akaomba aachiliwe huru.
Lakini hakimu alisema sharia imekataza mmoja kutoa matamshi ya kukejeli mtu mwingine kwa lengo la kusababisha taharuki na pia kuzua hali ya taharuki kwa lengo la kuvuruga Amani.
Alisema shtaka dhidi ya Waititu halina dosari na kuamuru ashtakiwe na ushahidi kuwasilishwa.
Bw Onyina alimwachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na kuamuru kesi itajwe Oktoba 9, 2024 polisi wamrudishie simu yake.