• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Likizo ya lazima kwa wakuu wa NCPB

Likizo ya lazima kwa wakuu wa NCPB

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wawili wa ngazi za juu katika Bodi ya Kitaifa na Mazao na Nafaka (NCPB) wameachishwa kazi kwa kuhusishwa na kashfa ya mahindi ambapo Sh1.9 bilioni zililipwa wafanyabiashara walaghai badala ya wakulima.

Jumatano kaimu mkurugenzi mkuu wa NCPB Albin Sang aliwaambia wabunge kwamba meneja mkuu anayesimamia Idara ya Fedha Cornel Ngelechey na meneja wa fedha John Gichuru walitumwa kwa likizo ya lazima.

Alisema hatua hiyo ilichukuliwa ili kutoa nafasi kwa uchunguzi sakata hiyo.

“Tulichukua hatua hiyo kwa sababu wakaguzi wetu wa masuala ya uhasibu walikuwa wakiendelea na wao. Vile vile, tuliwaalika wakaguzi kutoka nje kuchunguza kashfa hiyo. Wachunguzi hao walitumwa na Wizara ya Kilimo,” Bw Sang’ akaambia wabunge ambao ni wanachama wa kamati kuhusu uwekezaji.

Kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, pia iliagiza kwamba Mhasibu Mkuu Edward Ouko afanye ukaguzi maalum huru katika NCPB ili kuzuia kuwezesha kupatikana na “matokeo huru” katika shughuli hiyo.

“Tunasikitika kuwa mwezi mmoja baada ya sakata hiyo kufichuliwa, Wizara ya Kilimo haijamwalika mhasibu mkuu wa serikali kufanya uchunguzi wake. Tunaamuru hapa kwamba Mkaguzi Mkuu aitwe kufanya ukaguzi maalum kuhusu sakata hii ya mahindi kwa hatutaki pesa za umma kuendelea kupotea katika NCPB,” akasema Bw Nassir.

Mbunge huyo alisema kamati hiyo itaiandikia Wizara ya Kilimo kutaka kujua ni kwamba Afisi ya Mhasibu Mkuu haijaalikwa kuanzisha uchunguzi kuhusu sakata hiyo hata baada ya sakata hiyo kufichuliwa kwa umma.

Hata hivyo, Bw Peter Ringera ambaye ni mmoja wa wakaguzi kutoka afisi ya Mkaguzi Mkuu Edward Ouko alisema afisi hiyo haipokea ombi kutoka Wizara ya Kilimo ya kuitaka kuendesha ukaguzi maalum kuhusiana na sakata ya mahindi.

You can share this post!

Hatuwezi kutazama mamilioni ya mafuta yakifyonzwa KPC...

‘Watu wengi wataanagamia kwa vileo haramu, pombe...

adminleo