• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Maafisa 4 wa polisi wakamatwa kwa kukaidi agizo la Waiguru kuhusu pombe

Maafisa 4 wa polisi wakamatwa kwa kukaidi agizo la Waiguru kuhusu pombe

NA GEORGE MUNENE

MAAFISA wanne wa polisi wanazuiliwa kwa kukaidi agizo la Gavana Anne Waiguru kwamba baa zote zifungwe katika Kaunti ya Kirinyaga.

Watuhumiwa walikamatwa Jumapili na kuwekwa korokoroni katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru ili kuhojiwa.

Walipatikana wakibugia pombe katika baa moja baada ya Gavana Waiguru kuamuru vilabu vyote kufungwa kufuatia vifo vya watu 17 baada ya kunywa pombe haramu katika Kijiji cha Kangai.

Soma pia Jinsi ya kutambua pombe salama na ile itakayokuua au kukupofusha

Mnamo Jumamosi, Bi Waiguru aliamuru vituo vyote vya kuuzia pombe katika kaunti hiyo vifungwe na kufutilia mbali leseni zote zilizopatiwa vilabu hivyo ili kuruhusu mchakato mpya wa kuvipiga msasa.

Jumatano iliyopita, mtu mmoja zaidi alifariki na wengine wawili kupoteza uwezo wa kuona baada ya kunywa pombe yenye sumu katika kijiji cha Kandongu, Kirinyaga.

Inaaminika kuwa watatu hao walikunywa pombe iliyowekwa kemikali yenye sumu hasa baada ya kuanza kutapika na kulalamikia maumivu ya tumbo.

Walikimbizwa na majirani katika zahanati ya Kandongu hali zao zilipozidi kuwa mbaya, lakini mmoja wao alifariki akipokea matibabu.

“Tumempoteza mtu mwingine aliyetambulika kama Paul Mwai kwa pombe yenye sumu, hali ni mbaya,” alisema mmoja wa wakazi, Bi Jane Muthoni.

Soma pia Polisi 4 wanaodaiwa kuiba pombe yenye sumu na kuuzia mfanyabiashara wazuiliwa

Bi Muthoni alisema, Bw Mwai alikuwa jirani yake na kwamba alikuwa miongoni mwa waliompeleka hospitalini.

“Nilikuwa nyumbani nilipopata taarifa kuwa hali yake imekuwa mbaya baada ya kunywa pombe na mara moja tulimkimbiza hospitalini ila akaaga dunia,” alisema.

Wakazi waliojawa na hasira walishutumu polisi kwa kushindwa kukabiliana na watu wanaouza pombe yenye sumu katika eneo hilo.

Kisa hiki kinajiri siku chache baada ya watu wengine 15 kuangamia baada ya kunywa pombe yenye sumu katika kijiji cha Kangai.

  • Tags

You can share this post!

Taita Taveta katika ushindi wa mapema kwenye mvutano na...

Harusi haitoshi, kulingana na sheria, ndoa inathibitishwa...

T L