Maafisa wa KWS motoni kwa kuua mwanamume na kulisha mamba mwili wake
NA CHARLES WASONGA
MAAFISA sita wa Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Malindi kuhusiana na mauaji ya kikatili ya mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 50 Desemba 2018.
Kulingana na Afisa wa Upelelezi wa Jinai katika Kaunti ya Tana River Wycliffe Sifuna, sita hao wanatuhumiwa kumuua Bw Lami Bocha ndani ya Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki kisha wakatupa mwili wake ndani ya mto wenye mamba wengi wakautafuna.
Marehemu alipatikana akilisha mifugo katika mbuga hiyo kinyume cha sheria akiwa na wanawe watatu wa kiume.
Bw Sifuna alieleza kuwa baada ya wanne hao kukamatwa, maafisa hao wa KWS walimtesa na kumpiga risasi Bw Bocha. Kisha walirusha mwili wake katika mto Galana ulio na mamba wengi huku wanawe wakitazama.
Watoto hao walizuiliwa katika katika seli ya KWS mjini Voi.
Afisa huyo alisema kuwa kisa hicho kilitendeka mnamo Desemba 24, 2018 na kwamba wavulana hao ndio walitoa habari kuhusu mauaji ya baba yao kwa wakazi na polisi wa Garsen baada ya wao kuachiliwa huru mamo Desemba 28, 2018.
Maiti ya Bocha haikupatikana lakini polisi waliofika katika eneo la tukio walisema kuwa walipata maganda ya risasi zilizotumika, nguo zenye damu iliyokauka na glovu. Polisi walisema uchunguzi wa vitu hivi bado unaendelea.
“Ilitulazimu kuendesha shughuli ya kuwatambua washukiwa mjini Malindi badala ya Garsen kwa sababu wakazi wenye ghadhabu walikuwa wakitaka kuwashambulia maafisa hao wa KWS. Wavulana hao waliweza kuwatambua maafisa waliomuua baba yao na tukawakamata,” Sifuna akasema.
Aliongeza kuwa uchunguzi ulioanza Januari 2019 unaelekea kukamilika na kwamba washukiwa watafikishwa mahakamani hivi karibuni kushtakiwa kwa kuua kwa kukusudia.
“Tunakaribia kukamilisha kila hatua ya uchunguzi; tumefika katika eneo la tukio na kuchukua maganda ya risasi pamoja na vitu vingine vitakavyotumika kama ushahidi. Na pia inasemekana walitupa mwili wa mwanamume huyo ndani ya to Galana wenye mamba wengi,” Bw Sifuna akaongeza.
Mbunge wa Garsen Ali Wario alishutumu mauaji hayo na kuwataka polisi kuhakikisha kuwa washukiwa wameadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
“Hakuna mtu asiyeweza kukabiliwa na mkono wa sheria. Kwa hivyo, maafisa waliotekeleza kitendo hicho cha kikatili wanafaa kushtakiwa ili iwe funzo kwa wengine wenye hulka kama hiyo,” akasema Bw Wario.