Maafisa wa serikali waliohepa Mashujaa Dei pabaya
Na STEPHEN MUTHINI
KAMISHNA wa Kaunti ya Machakos, Abdillahi Galgalo amewashtumu wakuu wa idara mbalimbali za serikali waliokosa kuhudhuria sherehe za Mashujaa katika uwanja wa Kenyatta siku ya Jumamosi na kuwaamrisha kuandika maelezo na sababu zao za kukosa sherehe hizo.
Hata hivyo, Bw Galgalo aliyejawa na ghadhabu alisema hakuwa analenga kumnyanyasa yeyote katika hatua hiyo.
Pia alisema hana haja ya kuomba radhi kutokana na amri yake kwa kuwa ni wajibu wake kuhakikisha kwamba serikali inawakilishwa katika sherehe za kitaifa.
“Tunalipwa mshahara na serikali ili kuwahudumia raia na hatuna jingine ila kuwajibika. Kama mratibu wa shughuli za serikali katika kaunti hii sina haja ya kuomba msamaha na sijamnyanyasa mtu yeyote. Hata hivyo lazima wanieleze kwa nini walikosa kuhudhuria sherehe ya Mashujaa,” akasema Bw Galgalo.
Aidha aliwataka waajiriwa wote wa serikali kuiga mfano wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto ambao huhudhuria sherehe za kitaifa kila zinapoadhimishwa.
Mbali na sherehe ya Mashujaa iliyoandaliwa mjini Machakos mnamo 2016, sherehe ambazo zimekuwa zikufuatia zimekuwa zikikosa mvuto na kususiwa na viongozi wa kisiasa.
Gavana Alfred Mutua na viongozi wakuu wa kaunti vile vile walikosa sherehe za Jumamosi ambayo pia haikuhudhuriwa na mbunge wala diwani yeyote.
Hotuba ya gavana ambaye alikuwa katika sherehe za kitaifa Kaunti ya Kakamega ilisomwa na kamishna wa kaunti ndogo ya Machakos.
Rais Kenyatta aliongoza sherehe za kitaifa ambazo zilifanyika katika Uwanja wa Michezo wa Bukhungu. Rais wa Namibia pia alihudhuria sherehe hizo.