Maafisa wa usalama wanufaika na msaada wa chakula
Na LAWRENCE ONGARO
VIZUIZI vya magari barabarani vimesaidia sana kupunguza homa ya Covid-19.
Mnamo Jumatatu, maafisa wa polisi wanaozuia magari ya Machakos, na Murang’a eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki walinufaika na msaada wa chakula.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘ Jungle’ Wainaina, alizuru kizuizi hicho na kuwapa maafisa hao unga wa ugali, na wa chapati, barakoa, vieuzi, na macadamia.
Kizuizi cha Kilimambogo kipo katika eneo la makutano ya Kilimambogo, katikati ya barabara ya kuelekea Machakos na ya Matuu.
Bw Wainaina alisema ni vyema kutambua Kazi ngumu inayoendeshwa na walinda usalama hao na kwa hivyo alifikiria kuwajali na chakula.
“Ninaelewa kazi inayoendeshwa na maafisa hao ni ya kujitolea na kwa hivyo ni vyema kuwashukuru kwa njia ya kipekee,” alisema Bw Wainaina.
Aliwapa motisha kwa kuwahimiza waendelee kutumikia wananchi bila ubaguzi.
Wakati wa ziara hiyo, Bw Wainaina alielezewa jinsi kazi ya kizuizi inavyoendeshwa ambapo maafisa wa kituo hicho cha Kilimambogo walionyesha weledi wao jinsi ya kutumia kifaa cha droni ambacho hulenga kutafuta wanaopita njia za mikato.
Naibu kamanda wa polisi anayesimamia kikosi cha maafisa 20 katika kizuizi hicho Bi Monica Florence, alipongeza juhudi zinazoendelezwa na mbunge huyo kwa kuweka ushirikuano mzuri kati ya viongozi na maafisa wa usalama.
” Tunashuru msaada wa unga na vifaa vingine ulivyotupatia ambapo tunaona unatambua Kazi ngumu tunayofanya. Kwa upande wetu tunachukulia kama ni heshima kubwa kwetu,” alisema Bi Florence.
Alisema katika kizuizi hicho wanafanya Kazi kwa kupishana. Kuna wale wanaofanya mchana huku wengine wakichukua usukani usiku.
Alisema maafisa wa usalama hutumia kifaa cha Droni kufuatilia watu wanaopita njia za mkato ili kuhepa kizuizi.
“Kwa zaidi ya mwezi moja tumeweza kuwanasa wanabodaboda kadha ambao wengi wao huvukisha wasafiri kupitia mkato katika msituni,” alisema afisa huyo.
Alisema magari yanayoruhusiwa kupitia ni kama malori yanayobeba mizigo maalum, na magari madogo yaliyo na kibali iliyoruhusiwa kirasmi na wahusika.
Alisema wanaendesha kazi yao kwa njia inavyostahili bila kunyanyasa yeyote.
“Sisi kazi tunayofanya ni ya kuhakikisha tunazuia mienendo za mikato inayoendeshwa na watu tofauti. Kwa hivyo tunaendesha Kazi yetu kwa utaratibu unaostahili,” alisema Bi Florence
Alipongeza mpango wa serikali kuweka vizuizi katika maeneo tofauti kote nchi huku alisema imechangia pakubwa kudhibiti homa ya Covid-19.
Alisema katika eneo la Kiambu, kuna vizuizi vitatu muhimu ambazo ziko Maryhill kuelekea Gatundu kaskazini, lingene liko Blue- Post mjini Thika kuelekea kaunti ya Murang’a na hiyo ya Kilimambogo, iliyoko Thika Mashariki.
Alitoa ushauri kwa wananchi wasiwe na dhana potovu kuwa walinda usalama wananyanyasa watu kwenye vizuizi.
” Maafisa wa polisi hawana ubaya na mtu yoyote na iwapo mwananchi atatoa stakabathi zinazostahili bila shaka tutamruhusu kupita bila utata,” alisema afisa huyo wa polisi