• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maafisa wafanikiwa kunasa bangi na chang’aa katika nyumba moja mjini Thika

Maafisa wafanikiwa kunasa bangi na chang’aa katika nyumba moja mjini Thika

Na LAWRENCE ONGARO

POLISI mjini Thika wamefanikiwa kunasa bangi na chang’aa katika mtaa wa Kisii.

Kulingana na kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Thika Magharibi Bw Daniel Kitavi, bangi hiyo na pombe ya chang’aa ilipatikana ndani ya nyumba ya mshukiwa mmoja.

“Wakazi walimshuku jirani mmoja ambaye alifika akiwa kwa pikipiki alfajiri na kuingiza bangi hiyo chumbani mwake. Bila kupoteza muda majirani hao walipiga ripoti kituo cha polisi ili hatua ichukuliwe,” alisema Bw Kitavi.

Bangi hiyo inakadiriwa ni ya thamani ya Sh200,000 nayo chang’aa lita 10 ikinaswa katika nyumba ya mshukiwa huyo.

“Kulingana na wakazi wa eneo hilo ilidaiwa mnamo Jumatano, watu fulani walionekana wakibeba magunia kadha wakiingiza kwa nyumba ya mshukiwa mmoja aliyekuwa na bangi hiyo. Baadaye pikipiki mbili zilionekana zikitoka eneo hilo kwa kasi. Wakazi wa eneo hilo waliamua kupiga ripoti,” alisema Bw Kitavi.

Hata hivyo polisi walipofika kwa mshukiwa walipata tayari ametoweka lakini bangi hiyo ilipatikana kwa nyumba yake.

“Polisi walipofika walilazimika kuingia katika nyumba hiyo ambako walipata misokoto ya bangi imetiwa ndani ya magunia kadha huku pia chang’aa lita 10 ikipatikana kwa kibuyu kimoja,” alieleza Bw Kitavi.

Polisi walipopekua zaidi ndani ya nyumba, walipata vifaa ikiwemo ratili – ya kupimia bidhaa – ya kielektroniki, karatasi za sigara aina ya Rizla, na vifaa vingine vya kutayarisha bangi.

Wakati huo pia kitambulisho chake na cha mamake mzazi vilipatikana mle chumbani.

Bw Kitavi alisema tayari polisi wanamsaka mshukiwa huyo ambaye yuko mafichoni.

Wakazi wa mtaa huo wameshauriwa kushirikiana na polisi ili kumtafuta mshukiwa huyo.

Ripoti ya polisi inaeleza ya kwamba mshukiwa alitoka gerezani hivi karibuni ambako alitumikia kifungo cha miaka minane kabla ya kuachiliwa huru.

You can share this post!

Msikubali kutumiwa kutekeleza udhalimu, Ruto awarai polisi

Matiang’i afanya mabadiliko katika utawala wa mkoa