Habari Mseto

Maafisa wakuu Samburu wakana dai la ulaghai wa Sh84 milioni

April 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KARANI wa Kaunti ya Samburu, Bw Stephen Siringa na washukiwa wengine tisa walishtakiwa Ijumaa kwa kuidhinisha malipo ya Sh84.6 milioni kwa kampuni ya Gavana Moses Kasaine Lenolkulal kinyume cha sheria.

Bw Siringa aliyefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi jijini Nairobi, alikanusha shtaka la kuidhinisha Sh10,480,840 ili zilipwe Bw Lenolkulal.

Karani wa Serikali ya Kaunti ya Samburu Stephen Siringa Letinina akiwa katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Ijumaa, Aprili 5, 2019, jijini Nairobi. Picha/ Paul Waweru

Pesa hizi, upande wa mashtaka ulisema zilikuwa za kulipia mafuta ambayo kampuni ya Oryx Service Station ya Gavana Lenolkulal ilikuwa imeuzia kaunti hiyo.

Afisa mkuu anayesimamia masuala ya pesa katika kaunti hiyo, Bw Daniel Nakuo Lenolkirina, alishtakiwa kwa kumlipa Bw Lenolkulal Sh19,826,956 kama deni alilokuwa akiidai kwa kuiuzia mafuta kati ya Machi 2013 na Machi 2019.

Waziri wa Mazingira katika kaunti hiyo, Bi Josephine Namo alishtakiwa kwa kuidhinisha kuwa Gavana Lenolkulal alipwe Sh3,940,925 kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao walifunguliwa mashtaka pamoja na Bw Lenolkulal kwa kufanya njama kuilaghai kaunti hiyo Sh84,695,996 alizodai aliuzia mafuta kaunti hiyo.

Bw Lenolkulal aliyeshtakiwa mapema wiki hii aliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni.

Dhamana yake ilipunguzwa kutoka Sh100,000,000 pesa tasilimu aliyopewa alipokanusha mashtaka manne mbele ya hakimu mkuu Douglas Ogoti.

Wanaoshtakiwa kwa ulaghai huo ni Lenokulal, Lenolkirina, Lenasalia, Reuben Marumben Lemunyete , Linus Milton Lenolngenje, Paul Lolmuginani,Benard Ltarasi Lesurmat, Lilian Balanga, Andrew Ropilo Lanyasunya, David England Loosenge, Geoffrey Barun Kitewan na mfanyabiashara Hesbon Jack Ndathi.

Akiwaachilia kwa dhamana, Bw Mugambi alitaka kila mmoja wa washukiwa hao alipe dhamana ya pesa taslimu Sh10 milioni.
Endapo watashindwa kulipa dhamana hiyo, hakimu aliwataka watafute mdhamini wa Sh30 milioni.

Masharti hayo ya dhamana ni sawa na yale yaliyopewa Bw Lenolkulal na mahakama kuu.

Waliposhtakiwa mbele ya hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti, wakili Paul Nyamondi anayewatetea maafisa hao wakuu wa kaunti, alimtaka ajiondoe katika kesi hiyo akidai , “ana upendeleo na hisia zake kuwahusu washukiwa si njema ikitiliwa maanani alidai wanaotekeleza ufisadi hutenda makosa mabaya kuliko mauaji.”

Bw Mugambi aliamuru kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili, upande wa mashtaka ukitakiwa kueleza iwapo umewapa washukiwa nakala za mashahidi.