Habari Mseto

Maafisa wawili wa gereza wakamatwa na DCI kuhusu kifo cha mfungwa

January 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MACHARIA MWANGI

MAKACHERO kutoka kitengo cha DCI wamewakamata askarijela wawili kuhusiana na mauaji ya mfungwa katika gereza la Naivasha mnamo Juni 2019.

Taarifa kutoka kwa DCI ilisema kuwa waliwakamata sajini Dennis Wandati Masibo na afisa wa cheo cha konstebo Meriti Lansika maarufu kama Masai, baada ya uchunguzi kuhusu kifo cha mfungwa Simon Nduro Gitahi kutamatika.

“Wawili hao watashtakiwa kwa mauaji ya mfungwa kinyume cha sheria za nchi,” ikasema taarifa kutoka kwa mkuu wa DCI George Kinoti.

Mkuu wa Polisi wa Naivasha, Kenneth Njoroge alisema maafisa hao wawili wa gereza hilo walinyakwa na polisi Jumanne jioni.

Mwaka jana, idara ya magereza iliwasimamisha kazi maafisa hao wawili huku DCI na kitengo cha upelelezi cha HIU ,zote zikiendeleza uchunguzi sambamba kubaini iwapo walihusika na mauaji ya mfungwa huyo.

Afisa aliyekuwa akisimamia gereza hilo Mathew Mutisya pia alipewa uhamisho hadi makao makuu ya magereza na nafasi yake kupewa Samuel Ruto ambaye alikuwa akisimamia gereza la Industrial Area awali.

Kipigo

Tume ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR) nayo ilitoa ripoti iliyosema Bw Gitahi ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha maisha, alipigwa na kuteswa Juni 13, 2019, na askari hao wawili ambao walitwikwa jukumu la kumlinda.

Alifariki siku mbili baadaye na alihudumu kwenye gereza hilo siku moja pekee baada ya kuhamishwa kutoka lile la Kamiti.

Maelezo kwenye ripoti yao ilisema askarijela na wafungwa waliohojowa walikiri kwamba marehemu alipigwa kisha akafungiwa kwenye seli maalum ambako alinyimwa huduma za matibabu.