Habari Mseto

Maandalizi duni ya kesi ya NYS yafanya mahakama kulia hoi

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KUTOANDAA ipasavyo ushahidi katika kesi ya kashfa ya Sh226milioni iliyokumba shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) kumefanya mahakama inayosikiza kulia hoi.

Hata imebidi hakimu mkuu Douglas Ogoti na mawakili wanaowatetea washukiwa 37 walioshtakiwa kwa kufilisi NYS kuuliza , “ni kwa nini ushahidi huu hauajatayarishwa inavyopasa na washukiwa kupewa nakala zao.”

Bw Ogoti amesema tangu aanze kusikiza kesi hiyo amekumbana na vizingiti sio haba ambazo zimefanya kesi kuahirishwa kila mara.

Akasema Ogoti, “Kule nje itasemekana kuwa mahakama inachelewesha kesi.Tunalaumiwa bure. Sio mahakimu wanaochelewesha kukamilika kwa kesi hii.Ni afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma na ile uchunguzi wa jinai (DCI) zinazoyumbisha kusikizwa kwa kesi hii kwa kutowapa washukiwa nakala za ushahidi.”

Hakimu alidokeza wimbo ambao umekuwa ukikaririwa katika kesi hiyo ni mmoja tu – wa washtakiwa kutopewa nakala za mashahidi.

Washtakiwa na mawakili wao na hakimu wamekuwa wakiuliza swali moja nalo ni hili , “Mbona afisi ya DCI haitaki kuwapa washtakiwa nakala zote za ushahidi uliokusanywa na kurekodiwa kabla ya wao kushikiwa na kufikishwa kortini?”

Imebainika wazi wazi ni maafisa katika afisi ya DCI ambao wamekawia kuwapa washtakiwa nakala za ushidi waandae utetezi wao.

Katika muda wa zaidi ya mwezi mmoja kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kila inapoanza kusikizwa hata hakimu akasema DPP anakaidi haki za washtakiwa kwa kuchelewa kuwapa nakala za mashahidi.

Wiki hii kesi hiyo iliahirishwa mara mbili hata ikabidi Bw Ogoti kumwagiza afisa anayechunguza kesi hiyo afike mahakamani kueleza kuna ni.

Afisa huyo alifika na kuahidi kuwapa nakala za mashahidi ifikapo Alhamisi.

Haikuwezekana. Punde tu baada ya Bw Sebastian Mokua, shahidi wa kwanza kuingia kizimbani , alichomoa vocha ya malipo kwa makampuni ya Familia ya Ngirita ambao mawakili walisema “ hawajawahi kuuona.”

Tena Bw Ogoti alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bi Evah Kanyuira , “ Mbona hamjawapa washtakiwa nakala za ushahidi huu?”

Bi Kanyuira hakutoa sababu zozote ila kusema “ naomba ushahidi huu uwekwe kando ndipo washtakiwa wapewe nakala zao.”

Baada ya majimbizano ya muda tena ushahidi mwingine wa malipo ya makampuni Njewanga Enterprises na Ngiwaco Enterprises ulichomolewa.

Tena mawakili na hakimu walishangaa sababu ya DPP kuendelea kutoa ushahidi wa kuwatweza mioyo washtakiwa.

Bw Ogoti hakusita kumkemea DPP akisema anakaidi Kifungu nambari 50(2)(J) cha katiba kinachomtaka awape ushahidi wote washukiwa kwa muda unaofaa ndipo waandae ushahidi wao.

“Ukweli uliopo ndio huu, haki za washtakiwa hawa zimekandamizwan na DPP ikiwa kufikia sasa kuna ushahidi ambao hawajapewa,” alisema Bw Ogoti.

Baada ya uzembe wa DPP na DCI wa kutowapa washukiwa ushahidi kujianika adharani , ilibidi Bw Ogoti atoe maagizo mapya kwamba washtakiwa wote wapewe ushahidi ambao utawasilishwa dhidi yao ifikapo Desemba 6 2018

Ushahidi uliosababisha tumbo joto ulikuwa wa malipo ya Sh19milioni na Sh5milioni mtawalia kwa makampuni ya Njewanga Enterprises na Ngiwaco Enterprises.

Kampuni hizi zinazmilikiwa na Phyilis Njeria Ngirita na Lucy Wambui Ngirita.

Makampuni ya Familia hii ya Ngirita imedaiwa ilipokea mamilioni ya pesa kutoka NYS bila kutoa huduma.

Walioshtakiwa ni Anne Wambere Ngirita, Lucy Wambui Ngirita, Phyilis Njeri Ngirita na ndugu yao Jeremiah Gichini Ngirita.

Aliyekuwa katibu mkuu wizara ya ugatuzi Bi Lillian Omollo ameshtakiwa kuidhinisha malipo ya Sh54.8milion kwa Anne, Sh63.2m kwa Lucy , Sh50.9million na Phyilis  na Sh57.8million kwa Jeremiah kinyume cha sheria