Maandalizi ya Krismasi yashika kasi
Na WAANDISHI WETU
WAKENYA katika pembe tofauti za nchi wamezidisha maandalizi ya sherehe ikiwa imesalia siku moja tu kabla ya Krismasi.
Katika eneo la Pwani ambalo huvutia idadi kubwa ya watalii msimu huu, serikali imeweka mikakati ya kudumisha usalama.
Polisi wa usalama wa baharini wakishirikiana na polisi wa kawaida na maafisa wa Huduma za Wanyamapori watashika doria katika fuo za bahari.
Vile vile, bustani maarufu ya Mama Ngina Waterfront ambayo ilifanyiwa ukarabati uliogharimu Wizara ya Utalii Sh460 milioni itafunguliwa rasmi kwa umma hii leo.
Bustani hiyo iliyofunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta miezi miwili iliyopita ilifungwa wiki moja baadaye huku ukarabati ukiendelezwa.
“Watalii watakaokuwa wanaenda kuzuru ufuoni watatakiwa kuondoka sehemu hizo ifikapo saa kumi na mbili jioni. Msiende ufuoni usiku unaweza kuzama au hata kuliwa na wanyama wa baharini,” alisema mshirikishi wa eneo la Pwani Bw John Elungata, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya usalama eneo hilo.
Akiongea na wanabahari katika afisi yake katika jengo la Uhuru na Kazi, Kaunti ya Mombasa, Bw Elungata pamoja na Kamanda wa polisi wa eneo hilo Bw Rashid Yakub na naibu mkurugenzi wa shirika la wanyama pori nchini, Bw Author Tuda waliwahakikishia Wakenya usalama wao wanapozuru eneo la pwani.
Walisema sehemu hatari zitaongezwa maafisa zaidi ili kuzuia utovu wa usalama.
Mbuga za wanyama ikiwemo Kisite Mpunguti, Shimba Hills, Tsavo na Lamu pia zimepewa ulinzi mkali na maafisa wa wanyama pori.
Wakati huo huo, wafanyabiashara wa nguo mpya wamelia kupata hasara kwani wateja wengi wanageukia mitumba.
Bi Kaltun Abdhighafar muuzaji nguo za watoto katika soko la Marikiti mjini Mombasa, alisema tangu mwaka kuanza mauzo yamekuwa yakidorora kila uchao.
Hayo ni kinyume na wafanyibiashara wa nguo za mtumba katika soko la Kongowea mjini Mombasa, ambao wanaeleza kuimarika kwa biashara zao.
Bi Magdalena Muiruri aeleza kufuatia bei nafuu wanazouzia bidhaa zao,wateja wengi hupendela kununua mavazi katika soko hilo.
Katika Kaunti ya Nakuru, maafisa wa idara ya mifugo na wale wa afya ya umma wamezidisha juhudi za kukagua nyama wakati wa msimu wa sherehe za siku kuu ya Krismas na mwaka mpya.
Afisa mkuu wa afya katika kaunti hiyo Dkt Samuel King’ori, alisema maafisa wake wamezidisha doria katika vichinjio vyote ili kuhakikisha kwamba nyama ambazo wakazi wanatumia ziko salama.
Alisema kwamba maafisa hao watakuwa wakiandamana na maafisa wa usalama ili kuwakamata wale wote ambao watapatikana wakiuza nyama ambazo sio salama.
Aidha Dkt King’ori aliwaomba wakazi kununua nyama katika maeneo ambayo yanajulikana ili kuepuka magonjwa ya mifugo kama vile kimeta.
Winnie Atieno, Mishi Gongo, Samuel Baya na Erick Matara