Habari MsetoSiasa

Maaskofu wasema mkutano wa Ruto lazima ufanyike

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NDUNGU GACHANE na IBRAHIM ORUKO

Maaskofu katika Kaunti ya Murang’a wamesisitiza kuwa mkutano wa maombi ambao Naibu Rais William Ruto alipaswa kuhudhuria lakini ukaahirishwa dakika za mwisho utafanyika.

Kulingana na Askofu Stephen Maina wa kanisa la Full Time Winners Gospel Church, wanachama wa kamati inayopanga mkutano huo wamekamilisha maandalizi hata baada ya maaskofu wa Kanisa Kiangilikana na Kanisa Katoliki kujiondoa kutoka kamati hiyo.

Askofu Maina alisema licha ya maaskofu wawili wa ACK na Kanisa Katoliki kujiondoa, bado wataandaa mkutano huo. Aliongeza kwamba, ingawa walijiondoa, walitofautiana tu kimaoni lakini wako pamoja kama kanisa.

“Itakuwa makosa na kupotosha kusema kwamba kwa sababu maaskofu hao walijiondoa kutoka kamati ya maandalizi, kanisa limegawanyika, tumetofautiana kimaoni lakini tuko kanisa moja, unaweza kuwaona maaskofu hao katika mkutano huo wa maombi,” aliambia Taifa Leo kwa simu.

Mkutano huo utafanyika hata baada ya baadhi ya viongozi kudai ni wa kisiasa kwa lengo la kumtawaza Dkt Ruto kuwa chaguo la watu wa eneo la Mlima Kenya ili ajinufaishe kisiasa.

Mbunge wa Gatanga, Nduati Ngugi alikosoa mkutano huo wa maombi na kushangaa kwa nini viongozi wote wa Kaunti hiyo hawakushirikishwa na kualikwa.

Bw Nduati aliambia Taifa Leo kwamba, alifahamu kuhusu mkutano wa kwanza uliopaswa kufanyika Aprili 27 kupitia gazeti la Daily Nation na akashangaa kwa nini viongozi wote wa Murang’a hawakualikwa kuhudhuria.

“Huu haukuwa na ninaamini sio mkutano wa maombi lakini wa kisiasa unaolenga kumpigia debe Naibu Rais kwa sababu, ikiwa ni mkutano wa maombi wanavyodai, ningealikwa kwa sababu ninatoka Murang’a, na ni jirani ya eneobunge la Maragua utakaoandaliwa,” alisema.

Askofu Maina alisisitiza kuwa mkutano huo wa maombi sio wa kisiasa akisema hakuna mwanasiasa mwingine atakayeruhusiwa kuhutubu isipokuwa Dkt Ruto.

“Tutakuwa na viongozi 150 waliochaguliwa katika mkutano huo lakini ninakuhakikishia kwamba hakuna mwanasiasa atakayehutubu na ratiba itasimamiwa na viongozi wa makanisa,” alisema Bw Maina.

Aliongeza kuwa ingawa mapadri wa Murang’a wamesajili chama cha akiba na mikopo, masuala ya chama hicho hayatakuwa kwenye ajenda ya mkutano utakaofanyika Mei 11 kwa sababu sio wote watakaohudhuria ni wanachama.

Wakati huo huo, wanasiasa wanaomuunga Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga maarufu kama Kieleweke wataandaa mkutano wa kwanza eneo la Magharibi Jumamosi.

Seneta wa Kakamega Cleopha Malala alisema mkutano huo utafanyika katika uwanja wa Amalemba mjini Kakamega.

“Utakuwa mkutano mkubwa,” alisema Bw Malala. “Tunataka kuwapa watu wetu mwelekeo wa kisiasa na tunafikiri njia bora ni kuwaalika viongozi wengine ili tujue walivyofanya maeneo yao,” alisema.

Kinara wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi, mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi Cotu Francis Atwoli wanatarajiwa kuhudhuria.

Wengine ni mbunge maalumu Maina Kamanda, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, na mbunge wa Cheragany Joshua Kuttuny miongoni mwa wengine.