• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Mabadiliko katika NHIF yapingwa vikali

Mabadiliko katika NHIF yapingwa vikali

Na CECIL ODONGO

MUUNGANO wa Vyama vya Wafanyakazi Kenya (COTU) umepinga arifa iliyopendeza mabadiliko mapya kwa wanaokiuka kulipa ada zao za kila mwezi kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) na kutoa wito yasitekelezwe hadi mashauriano yaandaliwe.

Naibu Katibu Mkuu wa Cotu, Bw Benson Okwaro jana alisema mabadiliko yanayoangazia faini na kiwango kinachotozwa yatawaathiri Wakenya wengi ambao wamekuwa wakichangia bima hiyo, akisisitiza kuwa yaliafikiwa bila kuwahusisha viongozi wa Cotu.

Wiki jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa NHIF, Bw Nicholas Odongo alitangaza mabadiliko hayo aliyoyasema yatasaidia kukabiliana na wale wanaokiuka kanuni ya malipo ya bima hiyo na walaghai wanaoghushi stakabadhi za malipo.

Baadhi ya mabadiliko aliyoyapendekeza ni wanaojiunga na mpango huo hasa waliojiajiri au wanaotoka sekta kama Juakali kulipa Sh6,000 kisha kusubiri kwa miezi mitatu kabla ya kuanza kutumia kadi zao za NHIF.

Kwa wanaochelewa kulipa ada zao za kila mwezi, watahitajika kulipa riba ya asilimia 50 kwa kiwango chao kwa muda wa miezi 11. Pia watatakiwa kulipa ada za mwaka mmoja mbele kisha kusubiri kwa mwezi mmoja kabla ya kutumia kadi zao.

Ni masharti haya makali yaliyochochea Cotu kuandikia NHIF ikiirai ipange mkutano nao ili kuyatatua wakisema yanaumiza Wakenya huku wakiongeza kwamba huenda ni njama ya serikali ya kupata fedha zaidi kutoka kwa raia.

“Mabadiliko haya hayafai na yanalenga kuwakandamiza Wakenya ambao wanafanya juu chini kuhakikisha wanalipa ada zao za kila mwezi.

“Tunashuku kuna watu wanaoingilia wajibu muhimu ambao umekuwa ukitekelezwa na NHIF kwa lengo la kuipa sifa mbaya na pia kupata fedha zaidi,” akasema Bw Okwaro akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi.

Akiwa ameandamana na wanachama wa bodi ya Cotu, Bw Okwaro alisisitiza kuwa watatetea maslahi ya wafanyakazi wakati wa mkutano kati yao na maafisa wakuu wa NHIF na kuhakikisha mabadiliko hayo hayatekelezwi kamwe.

“Hatutalegeza kamba. Iwapo hatutaafikiana, basi tutawatangazia hatua ya kuchukua kwa sababu mabadiliko hayo yanaumiza wanaotoa pesa zao kila mwezi,” akaongeza.

Muungano wa Waajiri Nchini(FKE) pia umepinga mabadiko hayo, ukisema kwamba mashauriano hayakufanyika kabla yaafikiwe.

You can share this post!

Waliokuwa wakitegemea misaada ya Sonko waumia

Rungu la EACC laelekezwa kwa Ngilu

adminleo