Habari Mseto

Mabadiliko KDF ikiwa Mwathethe atastaafu Aprili

March 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na NYAMBEGA GISESA

MALUTENI Jenerali wanne wa jeshi ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kumrithi Mkuu wa Majeshi Nchini Jenerali (CDF) Samson Mwathethe ambaye huenda akastaafu Aprili iwapo muda wake wa kuhudumu hautarefushwa kwa miaka minne zaidi na amiri jeshi mkuu Rais Uhuru Kenyatta.

Mabadiliko yanayotarajiwa katika idara ya jeshi huenda yakamwathiri Naibu Mkuu wa majeshi Luteni Jenerali Robert Kibochi ambaye asipopandishwa hadhi na kumrithi Bw Mwathethe, atastaafu kwa kuwa amesalia tu na miezi michache kabla ya kuhitimu umri wa miaka 61.

Jenerali Mwathethe ni mwanajeshi wa pili kutoka kikosi cha wanamaji kuwa Mkuu wa Majeshi. Wa kwanza alikuwa Jenerali Joseph Kibwana.

Hali sawa na hii itamkumba Luteni Jenerali Leonard Ngondi ambaye kwa sasa anahudumu kama Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Muungano wa Afrika (UNAMID) wanaohudumumu Dafur, nchini Sudan.

Mabadiliko hayo pia huenda yakachangia uteuzi wa makamanda wapya kwenye vitengo vya jeshi la wanamaji, lile la wanahewa na lile la nchi kavu. Hata hivyo, hayo yatatokea iwapo Luteni Jenerali Walter Koipaton Ole Raria atapandishwa ngazi na kuwa Mkuu wa majeshi au Naibu mkuu wa majeshi.

Luteni Jenerali Kibochi na Ngondi wanawania kuwa nyapara wa KDF kwa kuwa mkuu mpya wa jeshi atatokea jeshi la nchi kavu kwa sababu Jenerali Mwathethe anatokea jeshi la wanamaji na mtangulizi wake Jenerali Julius Karangi alitokea jeshi la wanahewa.

Afisa mwengine wa ngazi ya juu jeshini ambaye pia yupo pazuri kuwa jenerali kamili ni Luteni Jenerali Adan Mulata.

Hata hivyo, kikwazo kwake pekee ni kwamba anatoka jeshi la wanahewa.

Vilevile ni vyema kuzingatia kwamba makamanda wa vyuo vya kijeshi mara nyingi hustaafu kutoka jeshini licha ya kushikilia nyadhifa za juu.

Ingawa haijajumuishwa kwenye sheria ya KDF, wadhifa wa mkuu wa jeshi umekuwa ukitolewa kwa mzunguko kwa vitengo vyote kwa muda wa miongo miwili iliyopita.

Mtindo huu ulikumbatiwa kama njia ya kumuenzi aliyekuwa mkuu wa majeshi Daudi Tonje na imesaidia kuzima uhasama au kampeni za chini kwa chini kwa wanaotaka kutwaa nafasi hiyo.

Iwapo atateuliwa kuwa CDF, Luteni Jenerali Kibochi atakuwa kamanda wa kwanza anayehusika na usimamizi wa kitengo cha mawasiliano kwenye jeshi la nchi kavu kusimamia kitengo hicho.

Kabla ya Jenerali huyo kuteuliwa kwenye cheo chake cha kisasa, aliwahi kushikilia vyeo katika karibu idara zote zinazohusika na jeshi.

Alihudumu kwenye kikosi cha Umoja wa Kimataifa kilichotumwa kuleta amani Sierra Leone kutoka 2000 hadi 2001.

Luteni Jenerali Ole Ria ambaye anatoka Kajiado Mashariki ndiye kamanda wa 21 wa jeshi la nchi kavu, wadhifa aliouchukua kutoka kwa Luteni Jenerali Kibochi.

Luteni Jenerali, Ngondi pia amewahi kuhudumu katika vitengo muhimu jeshini pamoja na kusimamia chuo cha kitaifa cha Jeshi na pia mkuu wa Jeshi la nchi Kavu kati ya vingine.