Macho kwa Rais mageuzi makuu yakinukia IEBC
Na PATRICK LANG’AT
MACHO yote sasa yanaelekezwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na uteuzi wa makamishna zaidi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) huku Naibu Rais William Ruto akianzisha malumbano mapya kati yake na hasimu wake mkuu wa kisiasa, kiongozi wa ODM Raila Odinga, kuhusu usimamizi wa taasisi hiyo.
Wiki jana, Bunge liliidhinisha mswada unaopendekeza kubuniwa kwa jopo la watu saba watakaotwikwa jukumu la kuteua makamishna wapya wa tume hiyo kujaza nafasi ya wanne waliojiuzulu miaka miwili iliyopita.
Wao ni; aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa IEBC, Connie Nkatha na makamishna Paul Kurgat, Margaret Mwachanya na Dkt Roselyne Akombe.
Kujiuzulu kwa wanne hao kumeacha tume hiyo chini ya usimamizi wa mwenyekiti Wafula Chebukati (pichani) na makamishna Profesa Abdi Guliye na Boya Molu.
Kuidhinishwa kwa uteuzi wa jopo litakaloteua makamishna wapya ndiko kulipelekea Dkt Ruto, wiki jana, kudai kuwa suala muhimu kwake sio atakayeongoza IEBC kwani mshindi ataamuliwa na wapiga kura.
“Hatuna shida na yule ataongoza IEBC. Tunachofahamu ni kwamba, mshindi katika uchaguzi wa urais ataamuliwa na wapiga kura. Wanaweza hata kumteua Oburu Odinga (Kakake Raila) kuwa mwenyekiti wa IEBC. Sijali. Kile ninachojua ni kwamba, hawawezi kuamua. Ni wananchi wataamua,” akasema Jumapili katika kaunti ya Embu.
Akaongeza: “Kile ningependa kuwaambia washindani wetu ni kwamba; mwaweza kuteua makamishna mnaowataka. Mwaweza kuwa na mwenyekiti wa IEBC mnayemtaka. Lakini tafadhali mtupe hakikisho kwamba wananchi watakapoamua mkubali matokeo na msisababishe fujo.”
Alisema hayo baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la Total Grace mjini Embu.
Jumatatu, Mbunge wa Belgut, Nelson Koech, mwandani wa karibu wa Naibu Rais, alisema Dkt Ruto alitoa kauli hiyo kutokana na dhana kwamba “mrengo ule mwingine ndio utakuwa na usemi katika uteuzi wa makamishna wa IEBC.”
“Huu mjadala kuhusu uteuzi wa makamisha wa IEBC unalenga kuendeleza dhana kuwa matokeo ya uchaguzi yataamuliwa na asasi hiyo wala sio wapigakura,” akasema.
“Baadhi ya watu wameingiwa na kiwewe kutokana na umaarufu wa Dkt Ruto na wanataka kuwatia woga wafuasi wetu kwamba licha ya umaarufu huo, hatima yake itaamuliwa na asasi ya IEBC. Hatutavunjwa moyo; tutaendelea kuwashawishi wapiga kura, kwani wao ndio muhimu,” akaongeza Bw Koech.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amepuuzilia mbali madai ya Dkt Ruto akisema hayana mashiko.
Amemtaka kujikita katika vita vyake na kiongozi wa chama hicho, Bw Odinga, wala sio Dkt Oburu.
“Oburu ni Mkenya kama wengine na anaweza kuhudumu katika wadhifa wowote nchini,” akasema Bw Sifuna.