Habari Mseto

Madai ya hongo na jinsi hakimu alijiondoa katika kesi ya ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HAKIMU mkuu wa mahakama ya Milimani Bw Lucas Onyina alijiondoa katika kesi ya ufisadi wa Sh7.9 milioni baada ya kufichua kwamba kuna mtu alijaribu kumhonga atoe uamuzi unaoegemea upande mmoja.

Mbali na ulaghai huo, afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekta Mkuu Eunice Njue alifichua kwamba polisi wamepokea madai kwamba Brian Reeves Obare amehusika katika ulaghai wa Sh89 milioni.

Inspekta Njue aliyewasilisha hati ya kiapo alielezea mahakama polisi wanaendelea kuandikisha taarifa za mashahidi kwa lengo la kumfungulia mashtaka zaidi.

Bw Lucas Onyinga alijiondoa katika kesi ambapo Obare ameshtakiwa kumlaghai Nancy Najira Odhungo Sh7,948,650 akidai atamtengenezea Visa za wasakakazi na wasomaji kusafiri hadi Canada.

Bw Onyina alijiondoa katika kesi hiyo Alhamisi Oktoba 31, 2024 na kuonya kwamba “mahakama haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wanaojaribu kuvuruga na kutweza haki.”

Hakimu huyo alichukua hatua hiyo ya ghafla alipokuwa anatarajiwa kutoa uamuzi ikiwa Bw Obare ataachiliwa kwa dhamana au la.

Mahakama ilikuwa imeombwa na kiongozi wa mashtaka Bi Nancy Kerubo imnyime Obare dhamana kwa vile akiachiliwa atatoroka.

“Huyu mshtakiwa alikuwa ametoroka kati ya 2022 na 2024,” Bi Kerubo alibaini.

Bi Kerubo alifichua kwamba Obare anau raia mara mbili. Ni Mkenya na vile vile ni Mshelisheli.

Alisema mshtakiwa ana vitambulisho vya Kenya na vile vile cha Ushelisheli.

“Endapo mshtakiwa huyu ataachiliwa kwa dhamana atatoroka. Amekwepa polisi kwa kipindi cha miaka miwili. Alitiwa nguvuni Oktoba 17, 2024 tangu 2022,” Bw Kerubo alisema.

Baada ya kujiondoa kwenye kesi hiyo kabla ya kutoa uamuzi, Bw Onyina aliamuru kesi hiyo isikizwe na hakimu mwandamizi Dolphina Alego.

Bi Alego aliombwa asimwachilie kwa dhamana kwa vile “hakuna uhakika kwamba mshtakiwa atafika kortini kuendelea na kesi.”

Hakimu alifahamishwa kwamba mshtakiwa alifunga afisi yake Nairobi aliyokuwa anafanyia kazi na kutoroka.

Wakili James Mochere anayemwakilisha Obare alisema mlalamishi katika kesi hii ni mshirika wake kibiashara na kwamba wana kesi katika mahakama kuu.

Brian Reeves Obare(kushoto) akiwa na wakili James Mochere kortini Oktoba 31 2024. Picha|Richard Minguti

“Huu ni mzozo wa kibiashara kati ya mlalamishi na mshtakiwa. Mahakama kuu bado haijaamua kesi hii,” alisema Bw Mochere.

Mahakama iliamuru mshtakiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Novemba 6, 2024 atakaporudishwa kortini uamuzi utolewe ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.

Pia aliagizwa apelekwe hospitali baada ya kudai ni mgonjwa.