'Madaktari wa Cuba watalipwa mishahara sawa na madaktari wa Kenya'
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI sasa inasema kuwa madaktari 20 kutoka Cuba waliowasili nchini Kenya Ijumaa jioni kupiga jeki vita dhidi ya Covid-19 watalipwa mishahara inayowiana na wenzao wa Kenya.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumamosi, Julai 18, 2020, alisema wataalamu hao wako nchini kubadilisha ujuzi na tajriba na madaktari wa humu nchini ambao wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga hilo.
“Hatutawalipa zaidi ya mishahara na malipo mengine tunayowalipa madaktari wetu. Nataka hili lieleweke vizuri. Hawa na madaktari wachache wenye ujuzi katika Nyanja mbalimbali za utabibu, na ambao wamekuja kutusaidia. Tutajifunza kutoka kwao na wao pia watajifunza kutoka kwetu,”akasema Bw Kagwe alipowahutubia wanahabari katika kaunti ya Embu.
Hata hivyo, Bw Kagwe hakutoa kiwango kamili cha mishahara na marupurupu ambacho madaktari hao watakuwa wakipokea kila mwezi kwa kipindi cha miezi sita ambacho watakuwa nchini.
Alieleza kuwa madaktari hao 20 watakuwa wakishirikiana sako kwa bako na wenzao wa humu nchini ili endapo kutatokea mlipuko mkali, wanaweza kuingilia kati.
“Vilevile, tunaendelea kuajiri madaktari wataalamu katika nyanja ya tiba ya magonjwa sugu kama kansa na kisukari. Hii ni kwa sababu kuna uhaba wa wataalamu kama hao nchini,” waziri Kagwe akaongeza.
Madaktari hao ambao wanatoka katika kikundi kinachojulikana kama Brigade of Henry Reeve; na wana ujuzi spesheli wa kukaliana na Hali ya Majanga na Milipuka ya Magojwa ya Kuambukiza.
“Tunatoa shukrani kwa serikali ya Cuba na Rais Miguel Diaz-Canel kwa kukubali ombi la Rais Uhuru Kenyatta na kutuma madaktari hao nchini Kenya,” waziri akasema.
Kenya imekuwa na ushirikiano mkubwa na Cuba katika nyanja ya utabibu ambapo imekuwa ikituma madaktari huko kwa mafunzo zaidi.
Na miaka miwili iliyopita Cuba ilituma madaktari wake 100 nchini Kenya kutoa huduma katika hospitali 94 za kaunti kote nchini.