Habari Mseto

Madaktari wa KNH walivyounganisha uume wa mvulana

January 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

MADAKTARI katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) wamefanikiwa kuunganisha sehemu ya uume wa mvulana aliyekatwa hadi ukatengana na mwili, baada ya kumfanyia upasuaji wa kina, katika kisa cha kipekee humu nchini.

Mvulana huyo wa miaka 16 alidaiwa kukatwa nyeti zake na wahuni wasiojulikana mnamo Desemba 18, saa saba usiku.

Mamake alimkimbiza hospitalini na kesho yake asubuhi akafikishwa katika hospitali ya KNH, ambapo alianza kuhudumiwa.

“Uume wake ulikuwa umekatwa unapochomoza kwa kutumia kisu cha jikoni. Alipofika, alikuwa akionekana mlegevu, mwenye uchungu na aliyekuwa ameshtuka,” akasema daktari aliyeongoza upasuaji wa mvulana huyo, Prof Kahinga.

Alisema baada ya huduma za haraka, timu ya madaktari 15 walianza kumfanyia upasuaji, na baada ya saa saba wakamaliza.

“Kuna sehemu kadhaa ndani ya kiungo hicho ambazo zilikuwa zimejeruhiwa na tukazirekebisha. Bahati yake ilikuwa kuwa alifika kwa muda mfupi baada ya kukatwa, matibabu ya aina hii hufanikiwa mtu anapofika hospitalini kwa haraka,” akasema daktari huyo.

Alisema walipokuwa wakimfanyia upasuaji, madaktari walilenga kuhakikisha kuwa mvulana huyo anarejesha uwezo wa kwenda haja ndogo, kupata nguvu za kiume tena na kuweza kuzalisha.

“Upasuaji huu ni wa kipekee sana na huchukua muda mfupi hivi kwamba mtu akiwazia kutafuta matibabu nje ya nchi, haitawezekana. Hawezi kufika huko kiungo chake kikiwa na uwezo wa kutibiwa tena,” Afisa Mkuu Mtendaji wa KNH, Dkt Thomas Mutie akasema.

Madaktari hao walisema kuwa visa vya wanaume kunywafuliwa nyeti vimeongezeka nchini, mbali na wale wanaokatwa wakiwa kazini na wengine wakitibiwa.

“Visa hivi si vya kawaida, lakini katika nchi yetu vimeanza kuwa vya kila siku,” akasema Prof Kahinga, akiongeza kuwa majuzi walimhudumia mgonjwa aliyekatwa nyeti na mkataji akazitupa.

Lakini walisema kuwa kwa mvulana huyo wa sasa, tayari ameripoti kuwa ameanza kupata nguvu za kiume, ishara kuwa upasuaji aliofanyiwa ulifanikiwa.

Madaktari sasa wanasema watazidi kufuatilia afya yake kwa wiki mbili zaidi, kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani.

Prof Kahinga alisema utoaji mafunzo ya upasuaji huo unaendelea kwa madaktari, ili kila kaunti iwe na angalau daktari mmoja mwenye ujuzi wa kufanya hivyo.