Habari Mseto

Madaktari walia Serikali haiwajali wakitoa matibabu

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

VALENTINE OBARA na WINNIE ATIENO

MADAKTARI na wahudumu wa afya wamelalamika kwamba, Serikali haijatilia maanani usalama wao wanapohudumia wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona.

Chama cha Wahudumu wa Afya nchini jana kilidai mwanachama wao mmoja tayari amethibitishwa kuambukizwa corona.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw George Gibore alisema mhudumu huyo wa kike aliambukizwa akiwa kazini na sasa kuna wasiwasi huenda alisambazia familia yake na wagonjwa wengine virusi hivyo.

Bw Gibore alisema kufikia sasa, wahudumu wa afya hawajapewa mafunzo maalumu kuhusu wanavyofaa kuhudumia wagonjwa wa virusi vya corona wala kupewa vifaa vya kutosha kujikinga kuambukizwa wakiwa kazini.

“Msimamo wetu ni kwamba, tuko tayari kujitolea lakini hatutajitoa mhanga. Hatutahudumia mgonjwa yeyote bila kujikinga. Pia, tunataka serikali itoe mafunzo kwa wahudumu wa afya kabla wiki mbili zikamilike,” akasema.

Kwa upande mwingine, madaktari walitaka serikali iwahakikishie kuwa endapo watafariki kwa virusi vya corona, familia zao zitalipwa fidia sawa na jinsi familia za wanajeshi hulipwa wakati mwanajeshi anapofariki vitani.

Chama cha Wahudumu wa Matibabu na Madaktari wa Meno (KMPDU) kilitilia shaka uwezo wa serikali kulinda madaktari na wahudumu wa afya walio katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Chibanzi Mwachonda alisema, kuna changamoto katika vita dhidi ya ugonjwa huo, ikiwemo uhaba wa vifaa vya madaktari kujikinga wanapokuwa kazini.

Dkt Mwachonda pia alisema mafunzo ya kutosha hayajatolewa kwa madaktari na wahudumu wa afya kuhusu jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa corona.

“Si madaktari wote wamefunzwa kuhusu hatua wanazopaswa kuchukua katika janga hili. Inafaa sote tuwazie kwa pamoja namna tutahakikisha hatutapatikana tukisinzia endapo kutakuwa na hali ya dharura,” akasema.

Alitaka serikali iimarishe utengenezaji wa vifaa vya kujikinga katika viwanda vya humu nchini kwani kuna uhaba kimataifa.

“Katika utoaji matibabu, hasa wakati wa janga kama ilivyo sasa, unahitaji kuzingatia usalama wako kwanza. Kama mhudumu wa afya ataambukizwa, ilhali yeye ndiye anategemewa kutibu mamia ya wagonjwa, hali itakuwa mbaya,” akasema.

Hata hivyo, alisema serikali kufikia sasa imeonyesha kujitolea kupambana na virusi hivyo lakini inafaa changamoto zote ziangaliwe kwa makini.

“Tumeshuhudia wahudumu wa afya wakifa katika mataifa mengine, na kuna walioambukizwa Ulaya na Asia. Tunataka kuwe na mfumo wa fidia ili daktari akiathiriwa, familia yake ilipwe ilivyo katika jeshi,” akasema Dkt Mwachonda.

Alitaka pia serikali iajiri wauguzi, madaktari na wahudumu wa afya zaidi.

Mapema wiki hii, Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alitangaza mpango wa serikali kuajiri wafanyakazi 1,000 wa sekta ya afya.

Lakini Dkt Mwachonda alisema, idadi hiyo bado haitoshi.

“Ni hatua nzuri na tunaisifu, lakini tunahitaji zaidi ikizingatiwa matarajio ya idadi ya maambukizi kuongezeka,” akasema.