Madaktari waonywa dhidi ya kuanika siri za wagonjwa mitandaoni
Na FRANCIS MUREITHI
MADAKTARI vijana wanaohitimu kutoka vyuo vikuu vya umma wameonywa dhidi ya kujadili hali za wagonjwa wao katika mitandao ya kijamii kwa sababu ni kinyume cha maadili ya taaluma yao.
Kulingana na Profesa Lukoye Atwoli wa Chuo Kikuu cha Moi, chochote ambacho madaktari hao wanachojadili au maoni wanayotoa, yanawaathiri wagonjwa na yanaweza kuhatarisha kazi yao.
Mhadhiri huyo alitoa onyo hilo Jumatatu katika bewa la Nakuru mjini la Chuo Kikuu cha Egerton wakati wa kula kiapo kwa madaktari 70 na wauguzi ambao walimaliza masomo yao.
“Ninataka muwe makini sana na mnachosambaza na kufichua katika mitandao ya kijamii kwa sababu chochote mnachosema kinachukuliwa kwa makini kwa kuwa madaktari ni watu wanaoheshimiwa katika jamii,” alisema Profesa Atwoli.
Alisema kama walinzi wa habari za siri za wagonjwa wao, madaktari wanapaswa kuhakikisha hazifichuki.
“Ni muhimu muwe waangalifu na mnachochangia katika mitandao ya kijamii na majukwaa mengine,” alisema.
Aliongeza: “Kufichua habari muhimu za wagonjwa wenu kunaweza kuwaathiri zaidi na kuwafanya wakose kupona,” alieleza Profesa Atwoli.
Alisema tabia yao katika mitandao ya kijamii na maeneo ya umma hufuatiliwa na Wakenya wengi na chochote kibaya kinaweza kusambazwa kwa wingi na kuharibu imani ambayo Wakenya wako nayo kwao kama madaktari.
“Iwe ni katika mitandao ya kijamii au maeneo ya umma, ni lazima madaktari wadumishe heshima na tabia nzuri na kuepuka kutoa habari ambazo zinaweza kutafsiriwa vibaya na kwa urahisi na umma,” alisema Profesa Atwoli.