Madaktari wataka marufuku ya kemikali ya kuhifadhi nyama
IRENE MUGO na AGGREY OMBOKI
MUUNGANO wa Madaktari wa Mifugo Nchini (KVA) sasa unaitaka serikali kupiga marufuku matumizi ya kemikali kuhifadhi nyama, ukisema kwa sasa hakuna mwongozo na sheria za kuidhinisha matumizi ya kemikali hizo katika sekta ya biashara ya mauzo ya nyama.
Kulingana na Mwenyekiti wa KVA Samuel Kahariri, serikali haina budi kuhakikisha maduka yanayopakia na kuuza nyama yanawekewa marufuku hadi sheria ibuniwe ya kulainisha sekta hiyo.
KVA ilisema kifungu cha Sheria ya Vyakula, Dawa na Kemikali ambacho kinaruhusu matumizi ya kemikali kuhifadhi bidhaa na vyakula hakizingatiwi na kinatumiwa vibaya na wafanyabiashara.
“Katika matukio ambayo kemikali ilitumika, bidhaa lazima zitiwe alama na kiwango cha kemikali kilichotumika kiwekwe ili watumiaji bidhaa wajiamuliwe wenyewe kabla ya kuzinunua,” akasema Dkt Kahariri.
Haya yanajiri baada ya runinga ya NTV kufichua jinsi wafanyabiashara laghai wamekuwa wakitumia kemikali kuhifadhi nyama ambayo wakati wake wa kutumika na binadamu umepita.
Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dkt Wekesa Masasabi akigusia suala hilo alisema, Wizara ya Afya imechukua nyama kutoka maduka mbalimbali ili kupimwa katika maabara ya kitaifa ya Afya ya Umma.
Dkt Masasabi pia alisema idara zote za afya ya umma katika kaunti mbalimbali zimeamrishwa kukagua supamaketi, vichinjio na kampuni za kuandaa na kutayarisha nyama pamoja na vyakula vingine kabla ya kuuzwa.
Lengo la ukaguzi huo ni kujua iwapo vituo hivyo vya mauzo vinatumia kemikali hatari kwa afya ya binadamu kuhifadhi nyama na vyakula vingine.
“Wizara ya Afya imekusanya sampuli za nyama zinazouzwa katika supamaketi mbalimbali ili kukaguliwa na kupimwa katika maabara ya kitaifa ya afya ya umma. Vile vile idara zote za afya kwenye kaunti zimeagizwa kuimarisha ukaguzi katika maduka ya kuuza nyama ili kufahamu iwapo kuna kemikali hatari zinazotumika kuhifadhi nyama,” akasema.