• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Madiwani Machakos wataka Spika awe Kaimu Gavana

Madiwani Machakos wataka Spika awe Kaimu Gavana

Na STEPHEN MUTHINI

MADIWANI wa Machakos sasa wanamtaka Spika wa bunge la kaunti hiyo Florence Mwangangi kutwaa wadhifa wa ugavana baada ya Mahakama ya Rufaa kufutilia mbali ushindi wa Dkt Alfred Mutua katika uchaguzi uliopita.

Walidai kuwa Dkt Mutua alikoma kuwa gavana wa kaunti hiyo Ijumaa  mahakama ilipobatilisha ushindi wake katika uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8, 2017.

Madiwani hao walisema uamuzi wa mahakama hiyo ya rufaa unafaa kuheshimiwa kwa sababu kufikia jana Dkt Mutua hakuwa amewasilisha notisi katika bunge la Machakos kuonyesha kuwa amepinga uamuzi huo katika Mahakama ya Juu, kama inavyodaiwa.

“Tumekutana bungeni kujadili hoja kuhusu hali ya usimamizi wa serikali ya Kaunti ya Machakos baada ya uchaguzi wa Mutua kufutiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa mnamo Ijumaa juma lililopita,” akasema MCA wa Ekalakala, Stephen Mwanthi.

Hoja hiyo ambayo ilidhaminiwa na Bw Mwanthi iliungwa mkono na madiwani 43 miongoni mwa jumla ya madiwani 59 wa bunge hilo.

“Kaunti ya Machakos imesalia bila gavana kulingana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa. Bunge hili halijapata ripoti yoyote kwamba Mutua amekata rufaa katika Mahakama ya Juu. Hivyo spika anafaa kuchukua mamlaka kama kaimu gavana hadi uchaguzi mdogo utakapoandaliwa,” akasema Bw Mwanthi.

Alisema shughuli za serikali ya kaunti hiyo haziwezi kusimama kwa sababu ya mtu mmoja.

“Ikiwa afisi imesalia wazi, spika anafaa kuchukua usukani huku tukisubiri Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itangaze tarehe ya uchaguzi mdogo,” akaongeza.

Madiwani hao walisema walifikia uamuzi huo kulingana na kipengee cha 182 (4) cha Katiba kinachosema kuwa spika wa bunge la kaunti anaweza kushikilia wadhifa wa ugavana endapo gavana ataondolewa afisini.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, Majaji wa Mahakama ya Rufaa, William Ouko, Mohammed Warsame na Kathurima M’Inoti walitoa uamuzi wa pamoja jijini Nairobi kwamba Dkt Mutua hakuchaguliwa kwa mujibu wa sheria.

“IEBC inaamuriwa kupanga uchaguzi mwingine wa nafasi ya gavana wa Kaunti ya Machakos kwa kuzingatia Katiba, Sheria ya Uchaguzi na kanuni husika,” kulingana na sehemu ya uamuzi huo.

Madiwani hao walisema wamempa Spika Mwangangi muda wa siku 14 afikie uamuzi kuhusu suala hilo kisha awasilishe ripoti katika bunge.

Akijibu hatua ya madiwani hao, Dkt Mutua alisema viongozi hao wamechochewa na mtu fulani kutoka nje ya kaunti hiyo ambaye analenga kuleta msukosuko katika usimamizi wake.

Alidai kuwa mamilioni ya pesa za ufisadi zimetumiwa kuwahonga madiwani hao na baadhi ya wabunge kutoka Ukambani ili kumpiga vita kisiasa kwa lengo ya kufifisha ndoto ya kuwania urais 2022.

Dkt Mutua alipoteza kiti hicho kwenye kezi ya rufaa iliyowasilishwa na aliyekuwa mgombezi wa kiti hicho kwa tiketi ya Wiper, Wavinya Ndeti.

Mara baada ya uamuzi huo alitangaza kuwa naye angekata rufaa katiika Mahakama ya Juu.

Iwapo uchaguzi huo utarejelewa, Dkt Mutua atakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Bi Wavinya Ndeti, ambaye anatarajia kuungwa mkono na wanasiasa wengi wa Wiper, ambacho ndicho chama kikubwa eneo la Ukambani.

You can share this post!

JAMVI: Ziara za Ruto zageuka siasa za 2022 licha ya...

RAMADHANI: Ni lazima maskini pia wapewe cha kusherehekea Idd

adminleo