Habari MsetoSiasa

Madiwani walivyopigana wakizozania kumng'oa Waiguru

June 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA GEORGE MUNENE

Purukushani ilizuka kati ya madiwani katika bunge la Kaunti ya Kirinyaga Jumanne wakati mjadala wa kumng’oa mamlakani Gavana Anne Waiguru ulipokuwa ukiendeshwa.

Madiwani hao walipigana asubuhi huku wakitatiza kikao hicho kwa muda lakini Sajini wa Ulinzi alirudisha utulivu kwenye kikao.

Matatizo yalianza pale diwani wa Mutira Kinyua Wangui alisema hoja ya kumtoa mamlakani Waiguru lazima ipitishwe.

Madiwani wawili wanaomuunga mkono Gavana Waiguru Bw Antony Munene (Karumandi) na Lucy Njeri alisimama na kudai kwamba sahihi zao zilikuwa ghushi kwani majina yao yalitokea kwenye orodha ya waliotaka Bi Waiguru atolewe mamlakani.

Wawili hao walikabiliana na Bw Wangui, wakiapa kwamba hawataruhusu mjadala huo uendelee.

Kulikuwa na machafuko kwenye kikao hicho huku madiwani hao wawili wakipiga kelele na kumpiga Bw Wangui. Hapo ndipo wenzao waliokuwa wakiunga mkono mjadaja huo walijaribu kuwatupa nje wawili hao na vita vikali vikazuka.

Makundi hayo mawili yalipigana na kurushiana mateke na kurushiana viti. Kulikuwa na mvutano kati ya pande hizo mbili, walikuwa wakiunga Gavana Waiguru na waliompiga uliopelekea Spika Bw Antony Gathumbi kusalia ameduwaa.