Madiwani wataka steji ziondolewe katikati ya jiji la Nairobi
Na COLLINS OMULO
MADIWANI wa Kaunti ya Nairobi sasa wanataka uongozi wa Nairobi Metropolitan Services (NMS), kuondoa maeneo ya maegesho na uchukuzi wa abiria katikati mwa jiji la Nairobi.
Madiwani hao wanadai kwamba waendeshaji wa magari ya umma wamegeuza barabara nyingi mijini na hata maeneo ya kutembea kama maegesho na sehemu za kuwabeba abiria bila kujali hatari iliyopo.
Kwenye mswada uliowasilishwa na diwani wa Woodley/Kenyatta Golf Course, Bw Mwangi Njihia, madiwani hao wanasisitiza kwamba uegeshaji magari kiholela kwenye barabara nyingi ndiyo umechangia ajali nyingi mjini haswa kugongwa kwa watu wanaotembea kando ya barabara.
Bw Njihia alitaja eneo linalopakana na Chuo Kikuu cha Nazerene jijini ambapo madereva wa magari ya uchukuzi wameligeuza pahala pa kuyaegesha magari yao na kuwabeba abiria bila kupokea idhini kutoka kwa kaunti.
“Magari ya PSV yanafaa yaruhusiwe kwa dakika chache tu mjini kuwabeba abiria na kuwashukisha wengine kisha yaelekee steji zao,” akasema Bw Njihia.
Diwani huyo anayehudumu muhula wake wa kwanza amehoji kwamba kuna maeneo ya kuegesha magari yanayohudumu kwenye barabara mbalimbali lakini madereva wake na hata wahudumu wa bodaboda hawajakuwa wakizingatia hayo na kukataa kimakusudi kuyatumia.
Hii ndiyo maana mwanasiasa huyo amemtaka Meja Jenerali Mohammed Badi kupitia afisi yake, ahakikishe magari yanaegeshwa tu katika maeneo yao.
Hata hivyo, alisema maeneo ya maegesho yalitengewa magari yanayohudumu katika barabara mbalimbali mara ya mwisho mnamo mwaka wa 2000 na kuna haja ya maegesho hayo kupanuliwa kwa sababu idadi ya magari ya uchukuzi imeongezeka maradufu miaka kadhaa baadaye.
“NMS inafaa kubuni sera maalum ya kutenga maegesho mapya au kuyapanua yaliyomo pamoja na vituo vya mabasi nchini,” akaongeza
Serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa miaka mingi imeshindwa kuzima tabia ya madereva wa magari ya uchukuzi wa umma kuyaegesha kiholela kwenye barabara za katikati mwa mji.
Mara nyingi tabia hii husababisha msongamano wa magari na
Gavana Mike Sonko mara nyingi amewaonya maafisa wa kaunti akidai wana tabia ya kupokea hongo kutoka kwa madereva hao kisha kuwaruhusu wayaegeshe magari yao maeneo yasiyofaa.
Mapema mwaka jana maafisa wa kaunti walitwaa magari 100 yaliyoegeshwa pasipofaa kwenye barabara za Tom Mboya, Moi Avenue, Latema, Munyu na karibu na Gill House.