Mafuriko yazidi kuleta maafa maeneo mbalimbali nchini
Na WAANDISHI WETU
SHULE tatu jana zilifungwa katika eneobunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu, huku maafa ya mafuriko yakiendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha tangu wiki iliyopita.
Wanafunzi katika shule za msingi za Kandaria, Ombaka pamoja na ile ya upili ya Kandaria walilazimika kurejea nyumbani, baada ya maji kujaa darasani na uga wa shule.
“Tumelazimika kuwatuma wanafunzi nyumbani kwa sababu madarasa yamejaa maji na vyoo vimesombwa. Kuna athari ya kuzuka kwa mkurupuko wa maradhi ndiposa tumewaagiza wanafunzi waondoke,” akasema mwalimu mkuu wa shule ya Kandaria, Bw John Mbeche.
Mbunge wa eneo hilo, Bw Jared Okello aliahidi kumfikia Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa ili wazuru eneo hilo na kutoa msaada kwa wakazi.
“Ninafahamu kwamba shule kadhaa zimefungwa kwa sababu ya mafuriko. Nawaomba wananchi wahamie maeneo ya juu salama ili kuzuia vifo, kwa sababu mvua inaendelea kunyesha na hali inatarajiwa kuwa mbaya hata zaidi,” akasema.
Aliongeza: “Pia nashirikiana na kaunti pamoja na serikali kuu kuhakikisha wakazi wameletewa misaada ya chakula, dawa na neti za kukinga mbu.
“Mafuriko yameathiri eneo hili kwa muda mrefu na lazima tutafute suluhu la kudumu.”
Mwanasiasa huyo pia alipendekeza wakazi watafutiwe ardhi kwingineko kwani Ziwa Victoria linaendelea kupanuka na maji yake kuenea hadi wanakoishi wananchi kila mafuriko yanatokea.
Katika eneo la Ukambani, wakulima wanaendelea kukadiria hasara kubwa baada ya mafuriko kuharibu mimea.
Taifa Leo ilibaini kwamba baadhi ya wakulima wamelazimika kuvuna mahindi yao hata kabla yakauke shambani.
Watu wawili walizama katika mto Muangini, Kaunti ya Makueni, siku ya Jumamosi.
Huko Pwani, shughuli za usafiri zilitatizika Taveta, Wundanyi na Mwatate baada ya barabara kufurika. Magari kadhaa yalikwama kwenye matope huku wasafiri wakikwama kwenye barabara ya Taveta-Njukini.
Wafanyabiashara walilalamikia hasara kubwa waliyopata baada ya bidhaa zao kuharibikia njiani.
“Tunategemea kilimo kulisha familia zetu lakini barabara sasa hazipitiki kutokana na mafuriko,” akasema mkulima Mathenge Kamuzu.
Ripoti za Cecil Odongo, Pius Maundu na Lucy Mkanyika