Magoha aonya Knut vikali kwa kupinga mtaala mpya
Na VALENTINE OBARA
WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, ameonya Chama cha Walimu Kitaifa (Knut) dhidi ya kukiuka sheria inapopinga utekelezaji wa mtaala mpya.
Knut imekuwa ikipinga utekelezaji wa mtaala huo kwa kisingizio kwamba hakujakuwepo maandalizi ya kutosha hasa kwa walimu, huku Katibu Mkuu, Bw Wilson Sossion akidai pia utekelezaji huo si halali.
Wakati serikali ilipoanzisha mafunzo kwa walimu wiki chache zilizopita, baadhi ya viongozi wa Knut katika maeneo mbalimbali nchini walijaribu kuvuruga shughuli hizo na kupelekea wengine wao kukamatwa wakashtakiwa mahakamani.
Mapema wiki hii, Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilisimamisha kazi kwa muda walimu 160 ambao walisemekana kutatiza shughuli hiyo ya kutoa mafunzo.
Walimu husika walipewa siku 21 kujitetea kabla iamuliwe kama watasimamishwa kazi.
Prof Magoha jana alisema kufikia sasa, wadau wengi katika sekta ya elimu wameonyesha kujitolea kwao kufanikisha utekelezaji wa mtaala huo wa umilisi na itakuwa vyema kama wanaopinga watatoa sababu zinazoweza kusaidia kuboresha changamoto wanazoamini zitadhuru ubora wa elimu.
“Tunapojitolea kujumuisha maoni ya wengine wakati wa utekelezaji, ni muhimu pia wao waheshimu misimamo ya wengine. Ninaheshimu walimu kwa sababu mimi ni mmoja wao. Kila mtu hufanya kosa na katika shughuli hii, pia mimi nitakosea lakini nitakubali makosa yangu na kujirekebisha,” akasema.
Alipokuwa akizungumza Ijumaa katika Kaunti ya Kakamega ambapo alikuwa anakagua utoaji wa mafunzo kwa walimu wakuu wa Magharibi kuhusu mtaala mpya, Prof Magoha alisema TSC ina haki ya kuadhibu walimu wanaokiuka maadili lakini bado kuna nafasi kwa walimu hao kusadiki na kuungana na serikali katika juhudi zake za kubadilisha mtaala.
Alifichua kuwa Wizara ya Elimu imepanga kukutana na Knut wiki ijayo kujadiliana kuhusu mtaala huo kwani tayari mikutano ishafanywa na wadau wengine ikiwemo Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET), Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA), Shirika lisilo la kiserikali la Elimu Yetu, na Chama cha Kitaifa cha Wazazi.
Wizara hiyo inalenga pia kukutana na viongozi wa kidini kwani madhehebu mengi yamewekeza katika elimu.
Kulingana naye, mkutano mkubwa wa wadau kitaifa umepangiwa kufanywa Agosti ambapo kutakuwa na utathmini wa kutosha wa hatua zilizopigwa na shida ibuka.