Habari Mseto

Magoha bado asisitiza shule zafaa kufunguliwa sasa

October 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha amesisitiza kuwa wakati umetimia kwa shule zote kufunguliwa.Mnamo Jumatatu, Rais Uhuru Kenyatta aliashiria kuwa Kenya bado haijajiandaa vilivyo kuhakikishia wanafunzi usalama wao dhidi ya virusi vya corona endapo itaamuliwa shule zifunguliwe hivi karibuni.

Akiongea jana alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kujibu maswali kadhaa kutoka kwa wabunge, Prof Magoha alionekana kusikitishwa na jinsi katika ukanda wa Afrika Mashariki ni Kenya pekee ambako shule hazijafuguliwa ilhali ‘sisi pia ni binadamu wa kawaida kama wenzetu kutoka mataifa jirani.

”Tanzania na Burundi hazikufunga shule zao. Mataifa majirani zetu kama vile Uganda, Malawi na Zambia yamefungua shule. Sisi pia tutafuata hivi karibuni,’ akasema.

Alitangaza kuwa shule zitafunguliwa baada ya wizara yake kutathmini hali itakavyokuwa baada ya kufunguliwa kwa vyuo vikuu kuanzia Jumatatu ijayo.

Prof Magoha alieleza kuwa watahiniwa wa mitihani ya KCSE na KCPE ndio wataripoti shule kwanza.

‘Tunataka kufuatilia hali itakavyokuwa baada ya hawa watu wazima kurejelea masomo ya kawaida kuanzia Oktoba 5, kabla ya kuamua ni lini wenzao wenye umri mdogo watarejelea masomo. Lakini ningetaka kuihakikishia kamati hii kwamba wakati umetimu kwa shule za msingi na upili kufunguliwa,’ akasema.

Kuhusu maandalizi kwa ufunguzi, waziri alisema wizara yake imepata misaada wa barakoa 700,000 kutoka kwa shirika la UNICEF huku Benki ya Kenya Commercial ikiahidi msaada wa barakoa milioni moja ambazo zitasambazwa katika shule za upili.