Habari Mseto

Mahakama yaelezwa jinsi ambavyo maiti zilipatikana

October 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAITI za wakili Willie Kimani, mteja wake na dereva wa teksi zilipatikana maafisa watatu wa polisi wa utawala wakihojiwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi (DCI), Mahakama Kuu ilifahamishwa Alhamisi.

Inspekta Mkuu Robert Owino alimweleza Jaji Jessie Lesiit kwamba alipashwa habari za kupatikana kwa maiti tatu katika Mto Athi akiendelea kuwahoji Inspekta Fredrick Lelimani, Sylvia Wanjohi, na Stephen Cheburet Morogo.

“Nilikuwa nimewashika Leliman, Morogo na Sylvia kuwahoji kuhusu kutoweka kwa Kimani, Josphat Mwenda na Joseph Muiruri nilipofahamishwa miili ya watatu hao imepatikana imetupwa mtoni Athi River eneo la Donyo Sabuk,” alisema Inspekta Owino.

Mahakama ilielezwa maiti za watatu hao zilikuwa zimetolewa na kupelekwa hadi mochari ya City kufanyiwa uchunguzi na kutambuliwa.

“Kwa hivyo hukuwa umejua miili imepatikana ulipowashika Leliman, Sylvia na Morogo mnamo Julai 1, 2016?” wakili Ombeta alimwuliza Insp Owino.

Na wakati huo huo Bw Ombeta anayewakilisha maafisa hao wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya Kimani, Mwenda na Muiruri aliomba mahakama isimwekee vizingiti anapomhoji Inspekta Owino.

Afisa huyo alisema alitwaa kutoka kwao bastola, pingu, simu zao za rununu na redio ya mawasiliano ya polisi mara tu alipowatia seli Leliman, Sylvia na Morogo.

“Nahisi hii mahakama inanikaba koo nisimwulize maswali afisa huyu kuhusu redio ya mawasiliano aliyokuwa nayo Leliman,” Ombeta akasema.

Wakili huyo alidai Jaji Lesiit alikuwa anamwekea viunzi katika utaratibu wa kuuliza maswali ya redio ya mawasiliano aliyokuwa nayo Leliman.

Hata hivyo Jaji Lesiit alijiondolea lawama na kumweleza Ombeta, “Ni wewe unajiwekea viunzi kwa kuuliza maswali kutoka kwa stetimenti ya afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Mlolongo badala ya kumhoji Inspekta Owino kuhusu ushahidi aliotoa afisa huyo aliyempa Leliman redio ya polisi ya mawasiliano.”

Mahakama ilifahamishwa OCS huyo wa Mlolongo alikuwa amempa Leliman mojawapo ya redio nne za mawasiliano ya polisi.

Redio aliyokuwa nayo Leliman iligunduliwa iliwasiliana akiwa mahakamani Mavoko, Mlolongo walikouliwa Kimani, Mwenda na Muiruri na pia katika eneo la Donyo Sabuk ambapo miili ilikutwa.

Leliman, Morogo, Sylvia, Sajini Leonard Maina Mwangi na kachero Peter Ngugi Kamau wamekanusha mashtaka ya kuwaua watatu hao mnamo Juni 23/24, 2016.

Inspekta Owino alikuwa akitoa ushahidi katika kesi hiyo alipoeleza jinsi ambavyo alitambua maafisa hao wa polisi ndio waliohusika na mauaji ya watatu hao.

Kesi inaendelea.