Mahakama yaikabidhi kampuni ya Njenga Karume shamba la Kiambu
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya Rufaa Ijumaa iliwapokonya wanachama 600 wa kampuni ya Gitamaiyu, Kiambu shamba lao la ekari 512 la thamani ya Sh3 bilioni na kuipeana kwa kampuni nyingine iliyohusishwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi marehemu Njenga Karume.
Kufuatia uamuzi huo wanachama wa Gitamaiyu wamewasilisha arifa katika mahakama ya juu wakisema “hatujaridhishwa na uamuzi huo wa mahakama ya rufaa.”
Majaji William Ouko, Asika Makhandia na Daniel Musinga walisema shamba hilo ni la kampuni ya Nyakinyua Mugumo Kiambaa ambayo mdhamini wake alikuwa mwanasiasa shupavu wa Kiambaa Bw Karume.
Familia ya Karume na wanachama wengine wa kampuni ya ununuzi wa mashamba ya Nyakinyua Mugumo Kiambaa ndio watakaofaidi na shamba hilo ambalo mzozo wa umiliki wake umekaa kortini kwa muda wa miaka 25.
Wanachama hao wa Gitamaiyu waliondoka mahakamani wakidodokwa na machozi kwa kupoteza shamba hilo ambalo wamelipigania kwa miaka 25 mahakamani.
“Tumeporwa adharani shamba letu tulilonunua kutoka kwa muwekezaji aliyemiliki kampuni ya Fanrose Limited Bi Norah Fangor kati ya 1974 na 1977,” wanachama wa Gitamaiyu waliambia Taifa Leo katika Mahakama ya Rufaa Nairobi Ijumaa baada ya kutolewa kwa uamuzi huo.
Kampuni maarufu ya ununuzi mashamba ya Nyakinyua Mugumo iliyohusishwa na Bw Karume na mkewe marehemu Wariara Njenga ndio walitangazwa kuwa wamiliki halisi wa shamba hilo.
Majaji William Ouko, Asike Makhandia na Daniel Musinga walitupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na wanacham hao wa Gitamaiyu.
“Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani wamiliki halisi wa shamba hili ni wanachama wa kampuni ya Nyakinyua Mugumo Limited,” walisema Majaji Ouko , Makhandia na Musinga.
Majaji hao walisema mzozo wa shamba hilo umekaa kwa muda mrefu mahakamani na “wapasa kufikia kikomo.”
Gitamaiyu ilikuwa imepinga uamuzi wa Jaji Aggrey Muchelule mwaka wa 2013 aliyesema shamba hilo lamilikiwa na wanachama wa kampuni ya Nyakinyua.
Wanachama wengi wa Gitamaiyu walikuwa wameajiriwa kazi ya kibarua kuvuna kahawa ya Norah.
Baada ya kuuza shamba hilo Norah alihamia Malindi alikofia.
Kwa miaka hiyo 25 walalamishi wamekuwa wakipambana na mbambe wa siasa na mwanasiasa maarufu marehemu Njenga Karume.
Bw Karume aliyekuwa na ushawishi mkubwa alidaiwa na wanachama hao wa Gitamaiyu kwamba alitumia uwezo na mamlaka yake kuwalaghai shamba lao.
Walalamishi walikuwa wameshtaki Nyakinyua Mugumo Co.Ltd, marehemu Karume na mkewe Wariara (marehemu pia), aliyekuwa Kamishna wa Ardhi J N Njenga. Msajili mkuu wa hatimiliki, Waziri wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu.
Wanachama hao wa Gitamaiyu walikuwa wanadai Bw Njenga alishirikiana na maafisa wakuu katika wizara ya ardhi kuwatapeli shamba lao.
Lakini wakili Francis Mwaura Shairi alitetea kampuni ya Nyakinyua Mugumo, Bw Karume na Wariara akisema walinunua shamba hilo na hakuwakughushi hati za umiliki wa shamba hilo.
Wanachama wa Gitamaiyu walikuwa wameililia Serikali ya hayati Mzee Jomo Kenyatta na marais wastaafu Daniel arap Moi na hata Mwai Kibaki kuwasaidia kupata shamba hilo wanalosema ni lao.
Wanachama hao wa Gitamaiyu wanasema wamezaliwa katika shamba hilo na wamelistawisha.