Mahakama yasifiwa kwa kuharamisha ushoga na usagaji
FARHIYA HUSSEIN NA LUCY NJESHURI
VIONGOZI wa Kiislaamu Jumamosi waliungana na Wakenya kupongeza Mahakama Kuu kwa kutupilia mbali kesi iliyolenga kuhalalisha ushoga huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakilaumu uamuzi huo.
Akizungumza na Taifa Leo mjini Mombasa, Katibu mratibu wa Baraza la Waislamu na Maimamu nchini (CIPK), Sheikh Mohammed Khalifa alisema Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa busara kwa kutupilia mbali kesi hiyo.
“Mahakama ilifanya jambo la maana kwani mambo hayo yanaleta laana na aibu kwa nchi yetu,” akasema Sheikh Khalifa.
Alisema dini ya Kiislamu inapinga vitendo vya ushoga na Kenya ni nchi ambayo inajulikana kuwa waumini wanapinga vitendo hivyo.
“Mungu alipotuumba alituumba tuwe jinsia mbili tofauti. Vitabu vyote vya kidini vinapinga mahusiano ya kijinsia moja,” akasema Sheikh huyo.
Aliwahimiza Wakenya kusimama imara na kujiepusha na vitendo kama hivyo kwani vinaweza kusababishia nchi laana na akawaomba waunge mkono serikali pamoja na mahakama.
“Dini zote, zinapinga vitendo hivyo kwani mafunzo yanakataza jambo hilo. Dini yetu inaamuru mtu anayepatikana akitenda ngono kabla ya ndoa, adhabu yake ni kucharazwa viboko 80 na anayeshiriki mahusiano ya kijinsia moja anastahili kutupiliwa mbali na kutengwa na jamii,” akasema Sheikh Khalifa.
Shirika la Human Rights Watch na Amnesty International zilikosoa mahakama kwa kudai uamuzi ulikandamiza haki za mashoga.