Habari Mseto

Mahakama zaanza kushughulikia kesi

June 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

SHUGHULI za kusikizwa kwa kesi katika Mahakama ya Milimani Nairobi zirejelewa Jumatatu baada ya kusitishwa kwa muda wa miezi mitatu.

Utaratibu mkali wa kuwakagua mawakili, washukiwa na kila mtu anayeingia katika jengo hilo uliwekwa huku mahema sita yakiwekwa kuwashughulikia wote waliofika kusikiza kesi.

Kila mtu alitakiwa kudumisha umbali uliotangazwa na wizara ya Afya na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wa mita moja unusu.

Eneo la maegesho ya magari lilitiwa alama ya rangi ya kijani kibichi. Waliofika kortini walipiga foleni kwenye sehemu zilizotiwa alama hiyo.

Huku hayo yakijiri, Kiongozi wa Wengi katika bunge le Seneti Samuel Poghisio alimtembelea Jaji Mkuu David Maraga katika Mahakama ya Juu.

Jaji Maraga na Bw Poghisio walifanya mashauriano lakini hawakuhutubia wanahabari.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Mwangi Gakuya azungumza na mawakili Karathe Wandugi na Danstan Omari (mwenye tai nyekundu). Picha/RICHARD MUNGUTI

“Bw Poghisio alikuwa amenitembelea tu kunisalimia,” Jaji Maraga alieleza wanahabari katika jengo la Mahakama ya Juu.

Bw Poghisio ambaye ni seneta wa West Pokot aliyeshinda kwa tikiti ya chama cha Kanu alifika katika afisi ya Jaji Maraga wiki moja baada ya hotuba kali aliyotoa kinara huyo wa mahakama akieleza mahangaiko aliyopata akitafuta nafasi ya kuzugumza na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu uteuzi wa majaji 41.

 

Kufunguliwa kwa mahakama tena kulitangazwa na Jaji Maraga wiki iliyopita akisema “shughuli za kusikizwa kwa kesi zitarejelewa chini ya utaratibu mkali.”

Hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi aliwahutubia mawakili, washukiwa na wananchi waliofika kortini na kuwaeleza , “lazima mwongozo uliotangazwa na Wizara ya Afya na shirika la afya ulimwenguni ufuatwe.”

Bw Andayi aliwaeleza  waliofika kortini  lazima kila mtu apimwe joto na kunawa mikono.