Majaji wakana madai ya kusaidia walanguzi
Na BENSON MATHEKA
CHAMA cha Majaji na Mahakimu wa Kenya (KMJA), kimetetea idara ya Mahakama dhidi ya madai kwamba majaji na mahakimu huwalinda walanguzi wa dawa za kulevya.
Chama hicho kilisema madai hayo yanalenga kufanya watu kukosa imani na mahakama ili wasiwe na pa kukimbilia kutafuta haki.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, rais wa chama hicho, Jaji Jacquiline Kamau, alitaja kisa cha waandamanaji waliomkabili Jaji Mkuu wakati wa kongamano la kila mwaka la majaji mjini Mombasa kama moja ya njama za kupaka tope idara ya mahakama.
Waandamanaji waliobeba mabango walienda katika ukumbi wa kongamano wakilaumu majaji kwa kuwa kizingiti katika vita dhidi ya mihadarati. Walidai kuwa majaji na mahakimu walikuwa wakiwalinda washukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya kwa kuwaachilia huru wakishtakiwa.
Hatua yao ilitokana na jinsi ilivyofichuliwa katika kesi ya Ibrahim na Baktash Akasha nchini Amerika, kwamba kuna majaji na mahakimu waliokuwa wakisaidia familia hiyo kwa biashara yao ya ulanguzi wa mihadarati, kando na watu wengine wenye ushawishi wakiwemo wanasiasa mashuhuri.
“Kilikuwa kitendo kilichopangwa kumfedhehesha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya aliye rais wa Mahakama ya Juu David Kenani Maraga,” alisema Jaji Kamau.
“Imeibuka kuwa maandamano hayo ya watu wasiojulikana, yalinuiwa kumharibia sifa Jaji Mkuu hasa kuhusu kesi za ulanguzi wa dawa za kulevya kwa kuonyesha ameshindwa kudhibiti idara hiyo,” aliongeza.
Alikanusha madai kwamba Jaji Maraga ameshindwa kusimamia idara ya mahakama hasa majaji na mahakimu wanaosikiliza kesi zinazohusu dawa za kulevya akisema yanapotosha.
“Ukweli ni kwamba amejitolea kuhakikisha kuwa majaji na mahakimu wote wanafanya kazi yao bila kuingiliwa,” alisema.
Aliwataka Wakenya kuheshimu wadhifa wa Jaji Mkuu kwa sababu anasimamia moja ya mihimili mitatu ya serikali inayostahili kulindwa.
“Kwa hakika, imani ya umma katika idara ya mahakama inaendelea kushuka kwa sababu ya mashumbulizi yaliyopangwa dhidi ya Jaji Mkuu, Majaji na Mahakimu yanayochochewa na baadhi ya watu katika jamii,” aliongeza Jaji Kamau.
Afisa huyo alihimiza umma kupuuza wanaolaumu mahakama akisema kuwa idara hiyo ndiyo kimbilio la mwisho la maskini mizozo inapozuka na wakapokandamizwa.
“Kenya inafuata njia hatari kwa kujaribu kuingilia uhuru wa mahakama kama inavyodhihirishwa na lawama zinazoelekezewa Jaji Mkuu David Maraga. KMJA inawaomba Wakenya wa nia njema kukataa na kupuuza madai haya ambayo yanatolewa na watu wasiolewa mfumo wa utendakazi wa mahakama,” alisema.
Aliongeza, “Sisi sote tuna jukumu la kuunga idara yetu ya mahakama ili kulinda utawala wa sheria. Matokeo ya kutofauta sheria yanaweza kudhihirishwa na yaliyotokea Kenya 2007 na 2008.”
Kauli ya KMJA inajiri siku tatu baada ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mombasa Edgar Kagoni kukamatwa akihusishwa na kutoweka kwa ushahidi katika kesi ya dawa za kulevya aliyoamua.
Bw Kagoni aliachiliwa huru baada ya Mahakama Kuu kuagiza asishtakiwa hadi kesi aliyowasilisha kupinga kukamatwa kwake iamuliwe.