Majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria yabomolewa Kisii
JADSON GICHANA na CHARLES WASONGA
MAAFISA wa Serikali ya Kitaifa na ile ya kaunti Alhamisi walibomoa majengo ambayo yamejengwa kinyume cha sheria mjini Kisii.
Shughuli hiyo iliyoanza Jumatano inaongozwa na idara ya mipango ya ujenzi na ustawi wa miji na inalenga majengo ya kibiashara ambayo hayajatimiza viwango vilivyowekwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi na Idara ya serikali ya kaunti kuhusu Mipango na Nyumba.
Zaidi ya majengo 100 yaliyojengwa kando ya kingo za mito, hifadhi za barabara, misitu, ardhi ya umma kama viwanja vya shule, pia yalibomolewa.
Baadhi ya majengo ambayo yalibomolewa ni jengo la ambalo wanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii hukodisha, maduka na nyumba nyingine ambazo zimejengwa kando ya Nyakomisaro.
Wengi wa wapangaji walijipata katika njia panda kwa vile hawakuwa wanajua kwamba majengo hayo yangebomolewa kwa sababu hawakujulishwa na wamiliki. Nyumba zilizobomolewa zinapatikana katika mitaa ya Mwembe, Daraja Moja, Nyambera, Daraja Mbili na katikati mwa mji.
Wale ambao nyumba zao ziliangushwa walionekana wakidondokwa na machozi kwa machungu ya kupoteza mali yao.
Wakati waziri wa Aridhi Faridah Karroney alifanya ziara mjini Kisii mwezi wa Februari 2, mwaka huu aliwaonya wastawishaji wote ambao wamejenga majengo kwenye chemichemi za maji kuyabomoa
Lakini inaonekana kuwa hawakufuata agizo hilo.