Habari Mseto

Maji ya Bahari Hindi yafurika na kuenea katika makazi Lamu

May 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

NYUMBA nyingi zilizojengwa karibu na ufuo wa Bahari Hindi katika mji wa kale wa Lamu hazikaliki baada ya maji ya bahari kufurika na kuenea katika makazi.

Mafuriko hayo yanayosababishwa na kufura kwa maji ya Bahari Hindi hushuhudiwa mara moja kila mwaka hasa kila wakati kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kinapowadia.

Shughuli za usafiri na biashara zimekuwa zikitatizika juma hili kwani sehemu nyingi zinazotumiwa hasa na waendeshaji pikipiki, punda na mikokoteni katika eneo la Huduma Centre, Ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Kituo cha Matibabu ya Punda, eneo la Bunge la Kaunti ya Lamu na pia sehemu yote iliyoko mkabala na ufuo wa Bahari mjini humo yote yakijaa maji.

Baadhi ya wakazi wamelazimika kuhama nyumba zao kwa muda baada ya makazi yao kusombwa na maji hayo.

Katika mahojiano na Taifa Leo mjini Lamu, mmoja wa viongozi wa kidini, Ustadh Ahmed Alwy, ameeleza kuwa kutapakaa kwa maji hayo ni jambo la kawaida ambalo wamekuwa wakishuhudia tangu zama za mababu zao.

Kulingana na Bw Alwy, kutapakaa kwa maji ya Bahari Hindi hadi kwenye makazi ya binadamu ni kiashirio kwamba Bahari imefura kutokana na wingi wa maji yanayosababishwa na dhoruba na upepo, hasa ule wa kusi.

Kiongozi wa kidini, Ustadh Ahmed Alwy, aeleza kuhusu hali ambapo maji ya Bahari Hindi yamekuwa yakifurika na kuenea hadi katika makazi kisiwani Lamu Mei 12, 2020. Picha/ Kalume Kazungu

Kiongozi huyo wa dini amesema wakazi wa Lamu, hasa Waislamu wamekuwa wakitumia hali hiyo ya kutapakaa kwa maji ya Bahari Hindi kila mwaka kutambua nyakati na majira fulani ya Mwaka wa Kiislamu.

“Mafuriko haya ya maji ya Bahari Hindi si jambo la kustaajabisha kwetu sisi wakazi wa Lamu. Mara nyingi hali hii hushuhudiwa hasa katika kipindi cha mwisho cha mwezi wa Shaaban katika kalenda ya Kiislamu, ambapo huo ndio mwezi unaokaribisha Ramadhani. Licha ya maji kutapakaa hadi kwenye nyumba zetu, sisi hatuna cha kuhofia kwani baada ya muda maji hayo hupungua yenyewe,” akasema Bw Alwy.

Naye Bw Mohamed Abdulkadir amewasisitizia Waislamu na wakazi wote wa Lamu waombe kila mara msimu huo wa kushuhudiwa kwa maji ya mafuriko kutoka baharini hapo kisiwani Lamu.

Kulingana na Bw Abdulkadir, maji hayo mara nyingi huashiria neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

“Sisi wakazi wa Lamu huichukulia hali hii kuwa ni baraka kutoka kwa Mungu. Hii ndiyo sababu kila mara mafuriko hayo yanaposhuhudiwa, sisi viongozi wa kidini huwahimiza sana waumini kumuwelekea Mwenyezi Mungu na kuomba ili heri na neema zisipotee kwetu,” akasema Bw Abdulkadir.