• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:50 AM
Makahaba watua Kiambu kunyonya Sh1.6 bilioni za fidia kwa wakazi

Makahaba watua Kiambu kunyonya Sh1.6 bilioni za fidia kwa wakazi

Na MWANGI MUIRURI

MAKAHABA wamevamia eneo la Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu kwa nia ya kuvuna sehemu ya Sh1.6 bilioni zinazotarajiwa kulipwa wakazi kuanzia Jumatano.

Fidia hiyo ni kwa wakazi watakohamishwa kwenye mashamba yao kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Kariminu.

Kulingana na mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mikahawa katika Kaunti ya Kiambu, Philemon Mwaniki, vyumba vya malazi katika eneo hilo vimeshuhudia ongezeko la wateja wapatao 1,200 tangu wikendi.

“Biashara ya lojing’i imeimarika katika vituo vya biashara vya Gituamba, Githobokoni, Chania na Mang’u. Wengi wa wateja ni wanawake tunaoshuku ni makahaba,” akasema.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Gatundu Kaskazini, Bi Wanjiku Kibe, makahaba hao walianza kuingia eneo hilo baada ya kupata habari kuwa kuanzia kesho wakazi wataanza kulipwa fidia ili waondoke katika mashamba yao.

“Wengi watalipwa kati ya Sh5 milioni na Sh40 milioni. Familia hizo zisipopanga vizuri jinsi ya kutumia pesa hizo, fidia hiyo inaweza kugeuka kuwa janga. Ombi langu ni kwa wakazi hasa wazee kutumia pesa hizo kwa makini kwa manufaa ya familia zao,” akaeleza Bi Kibe.

Alipotangaza kuhusu kuanza kulipwa kwa fidia hiyo, Waziri wa Maji, Bw Simon Chelugui aligusia suala hilo:

“Masikitiko yangu ni kuwa nimeona miradi kama hii ikigeuka kuwa balaa kwa familia nyingi. Nimeona familia zikilipwa fidia naye shetani anaingia ndani ya bongo za baadhi ya wazee ambao wanatoweka nyumbani na kufuja pesa hizo zote mitaani.

“Ninajua kuwa kunao wataanza kutafuta mabibi zaidi wa kuoa na wengine wa kula raha nao. Ombi langu ni kuwa pesa hizi ziwasaidie kujijenga lakini zisibomoe familia zenu.

“Ningeomba viongozi wa hapa Gatundu wawasaidie wakulima hawa kwa kuwatafutia wataalamu wa kuwapa mawaidha ya kutumia pesa hizo. Wengine watakimbia kununua magari ya kifahari huku wengine wakiingia mitaani kula raha,” akasema Bw Chelugui.

Alisema kuwa familia nyingi zilikataa kutafutiwa makao mbadala na kujengewa nyumba na badala yake zikaamua kupokea pesa taslimu.

Kamanda wa polisi wa Kiambu, Adiel Nyange alisema kuwa maafisa wake wako tayari kuwaandama wote watakaonaswa mitaani wakishiriki ukahaba ama kuwaibia wakazi kwa kuwawekea dawa za usingizi kwenye vinywaji.

“Hata ikiwa kazi ya polisi sio ya kuchunga watu wazima, tutajimudu kuokoa hali kadiri ya uwezo wetu. Wahudumu wa baa pia sharti wawe makini kuhakikisha usalama wa wateja wao,” akasema Bw Nyange.

You can share this post!

Polisi wakana kushirikiana na wanamgambo wa Al-Shabaab

Huduma Centre ya Thika sasa kuhudumia wananchi kuanzia...

adminleo