Malaika aliyeponea kifo Solai ampa mamaye tabasamu
NA PETER MBURU
ALIPOOKOLEWA na wasamaria wema kutoka ziwa la matope baada ya mkasa uliosababisha vifo vya watu 47 Solai, hakuna aliyedhani kuwa Patrick Wekesa, mtoto wa umri wa miezi miwili angekuwa hai.
Akiwa amegubikwa na matope mwili wake mzima, usoni kote na povu mdomoni, wengi walikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa hakuponea mawimbi hayo ya kifo.
Hata hivyo, sekunde chache baadaye, alianza kutoa povu na kulia nao waokoaji wakatabasamu baada ya kubaini kuwa kwa kweli malaika alikuwa hai, alipigana kwa hali na mali kuishi.
Dakika chache baadaye alipofikishwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Bahati, wauguzi walikuwa na hali ngumu kubaini ikiwa jinsia ya malaika.
“Alikuwa amegubikwa na matope katika mwili mzima, kuiongezea vidonda usoni, mikononi na miguuni,” akasema Bi Jane Wanyoike, msimamizi wa wahudumu katika hospitali hiyo.
Kinaya cha pili kilikuwa kuwa waliomfikisha hospitalini walisema mamake alikuwa ameaga, baada ya kumpata akiwa amezirai.
Walimpata mtoto akiwa amefungwa mgongoni, lakini mama akiwa amepoteza fahamu.
“Mtoto aliletwa hapa akiwa peke yake, lakini baadaye tukabaini kuwa mamake alikuwa uhai baada ya kufikishwa hapa kwa matibabu. Baada ya kuwahudumia tuliwaunganisha,” akasema Bi Wanyoike.
Wekesa, mtoto aliyesherehekea miezi miwili baada ya kuzaliwa akiwa hospitalini aliokoka kifo kwa tundu la sindano, lakini akagharamia kupigania uhai kwa alama zilizomjaa usoni, kuelezea tu hali aliyopitia.
“Ndiye mtoto wa pekee niliyebakishiwa na mkasa huo ambao uliwaangamiza watoto wangu wawili, sikuamini kuwa niyeye aliyepenya kwani ni jambo ambalo sikutarajia kabisa,” akasema Bi Jane Akur, mamake malaika huyo.
Ulipotokea mkasa, nia yake ilikuwa kuwaokoa watoto wake wote, lakini uzito wa mawimbi ulipozidi, walitengana na wakubwa wawili pamoja na bwanake.
Bi Akur alijeruhiwa vibaya, lakini kama zawadi ya mwenyezi mungu akabakishiwa malaika Wekesa kumfuta chozi.
Mumewe pia aliponea, japo na majeraha aliyotibiwa hospitalini na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
“Siku iliyofuata nilifanyiwa upasuaji na baadaye nikaunganishwa na mtoto wangu, sikuamini ni huyu aliyepona. Alikuwa mdogo sana na matarajio yangu hayakuwa kuwa angepenya,” akasema mama huyo.
Lakini hata alama za vidonda zikimjaa usoni, mtoto wekesa bado ni mwenye furaha tele, nguvu na hata akiwa hospitalini bado anampa mamaye tabasamu maishani.