• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
Malala amchemkia Oparanya kwa kupuuza vijana

Malala amchemkia Oparanya kwa kupuuza vijana

Na SHABAN MAKOKHA

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala amemshutumu Gavana Wycliffe Oparanya kwa kukosa kuwajumisha vijana na walemavu kwenye mabadiliko ya baraza la mawaziri aliyoyatekeleza wiki iliyopita.

Bw Malala amesema Gavana huyo amekuwa na mazoea ya kuwateua wakongwe kwenye nyadhifa mbalimbali katika kaunti hiyo ilhali kuna vijana wenye ujuzi ambao wanafaa kuwajibikia kazi hiyo.

“Unatarajia vijana wapate uzoefu kutoka wapi iwapo hujawapa kazi serikalini? Gavana Oparanya hajazingatia yaliyomo kwenye katiba kwa sababu serikali yake haina hata mlemavu mmoja,” akasema Bw Malala.

Seneta huyo wa chama cha ANC sasa ametoa wito kwa Bw Oparanya kubadilisha uteuzi wa juzi na kuwapa vijana na walemavu nafasi katika utawala wake.

Vuguvugu la vijana wa Mulembe ambalo linawawakilishi kutoka kaunti zote za Magharibi, hivi majuzi liliteua Seneta huyo kama msemaji wao kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

Bw Malala pia amemsifu gavana huyo kwa kumpokonya Naibu wake Profesa Philip Kutima wizara ya kilimo japo akataka nafasi hiyo ipokezwe kwa kiongozi kijana.

Hata hivyo, madiwani Joel Ongoro (Kisa Mashariki) , Geofrey Ommatera (Kisa ya Kati) na Moses Swaka (Kisa Kaskazini) wa ODM wameungana mkono mabadiliko yaliyotekelezwa na gavana huku wakimshutumu Bw Malala kwa kuzembea kupigania maslahi ya vijana kitaifa.

You can share this post!

Wakuzaji miraa walia Somalia ikizuia ndege yenye tani 11...

WANDERI: Ghasia za Nakuru zizimwe kabla ya hali kuzorota...

adminleo