• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Malala, Echesa walivyonaswa

Malala, Echesa walivyonaswa

Na BENSON AMADALA na VALENTINE OBARA

VIOJA vilishuhudiwa Ijumaa wakati Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa walikamatwa na wapelelezi kwa kuhusishwa na uhalifu ambao umesababisha maafa kwa wakazi wa Kaunti Ndogo ya Matungu, Kaunti ya Kakamega.

Bw Malala alikuwa katika hoteli iliyo Kisumu wakati wapelelezi walipomnasa mwendo wa saa tisa mchana.

Ilifichuka kwamba wapelelezi hao walienda katika Hoteli ya Sovereign wakiwa kwenye magari mawili, wakamshika Bw Malala, lakini akajaribu kujinasua kutoka mikononi mwao bila mafanikio.

Alipelekwa moja kwa moja hadi katika makao makuu ya polisi ya eneo la Magharibi, Kaunti ya Kakamega kuhojiwa.

Dakika chache kabla ya saa kumi na mbili jioni, Bw Echesa naye alijisalimisha katika kituo hicho cha polisi.

Bw Echesa alikuwa amehudhuria hafla iliyoandaliwa na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale katika eneo la Malinya, Kaunti ya Kakamega ambayo ilihudhuriwa pia na Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Alikaa hadi hafla ikakamilika, akaondoka kwenye msafara wa Dkt Ruto, na inaaminika baada ya hapo alielekea kwa polisi kujisalimisha.

Lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya wafuasi wa wanasiasa hao wawili wenye ushawishi mkubwa kwa vijana eneo la Magharibi, kuanza kukusanyika katika kituo hicho.

Hali hii ililazimu maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia kuweka ulinzi langoni mwa kituo hicho.

Baadaye, ilibidi wawili hao wapelekwe katika Makao Makuu ya Polisi wa Nyanza yaliyo Kisumu ili kuzuia mtafaruku katika kituo cha Kakamega.
Kamanda wa Polisi wa eneo la Nyanza, Bw Vincent Makokha, alithibitisha kwamba wawili hao walikuwa kituoni humo.

Katika Kaunti ya Kakamega, Diwani wa Wadi ya Mayoni, Bw Libinus Oduori pia aliitwa kwenda kuandikisha taarifa kuhusu visa hivyo vya mauaji.

Wapelelezi walisema wanasiasa hao wanachunguzwa kwa uchochezi na kutoa usaidizi kwa vijana walio katika magenge ya wahalifu ya 42 Brothers na 14 Brothers.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kakamega, Bi Wilkister Verah, wanasiasa hao waliitwa kuandikisha taarifa kuhusu uhalifu dhidi ya umma unaotendwa na magenge ya wavamizi wanaotumia silaha kama vile panga.

“Tuliwaita wanasiasa hao kuwahoji kufuatia agizo la Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kwamba kila mmoja anayehusishwa na visa vya Matungu afanyiwe upelelezi,” akasema Bi Verah.

Polisi walisema kuna wanasiasa wengine ambao wanatafutwa kuhusiana na visa hivyo.

Operesheni kali

Mnamo Alhamisi, Dkt Matiang’i alitangaza operesheni kali ya usalama alipozuru eneo hilo, akaonya viongozi wanaodaiwa huchochea uhalifu.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, wakuu wa usalama na viongozi kutoka ukanda wa Magharibi.

Kabla ya Dkt Matiang’i kufanya ziara hiyo, wahudumu wa bodaboda walikuwa wameanza kuchukua hatua mikononi mwao kwa kuangamiza washukiwa wa uhalifu.

Bw Malala ambaye ni mwanachama wa Amani National Congress (ANC) na pia Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti, amepata umaarufu Kakamega kwa ukakamavu wake wa kisiasa.

Ingawa ni mwanachama wa ANC, Bw Malala ambaye anatumikia useneta kwa mara ya kwanza, amejitokeza kuwa mtetezi mkubwa wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Kwa upande mwingine, Bw Echesa alijizolea umaarufu Magharibi alipokuwa Kiongozi wa Vijana wa ODM kwa muda mrefu, kabla ya kuhama chama hicho na kuungana na Dkt Ruto katika Jubilee na kuonekana kuwa mkosoaji mkubwa wa Bw Odinga.

Ijumaa, hali ya utulivu ilikuwa imeanza kurejea katika eneo hilo, siku moja baada ya serikali kuwatuma polisi wa GSU kuyafurusha magenge ya wahalifu ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi.

RIPOTI ZAIDI: Victor Raballa na Shaban Makokha

You can share this post!

Malkia Strikers yatua Uganda baada ya nuhusi ya kusubiri...

KENYA CUP: KCB yadunga Kabras Sugar mwiba mchungu katika...

adminleo