Malipo ya feri mpya yaibua utata
Na MOHAMED AHMED
UTATA unazidi kukumba malipo ya ziada ya Sh300 milioni kwa ajili ya uundaji wa feri ya pili iliyonunuliwa na serikali, huku maafisa wa kampuni ya Uturuki iliyopewa kandarasi ya ujenzi huo, wakitarajiwa humu nchini kuihimiza serikali ilipe pesa hizo.
Wanakandarasi hao kutoka kampuni ya Ozata Shipyard ya Uturuki, wanatarajiwa humu nchini Jumatatu wiki ijayo kudai pesa hizo ili kuweza kuleta feri hiyo ya Mv Safari.
Feri hiyo ya Mv Safari ni miongoni mwa zile mbili zilizonunuliwa na serikali kwa thamani ya Sh2 bilioni kutoka Uturuki. Feri nyingine ni ile ya Mv Jambo.
Kampuni hiyo ilileta feri ya Mv Jambo pekee humu nchini Agosti 2017 na kusalia na ile ya Mv Safari ambayo kuletwa kwake kulicheweshwa na kesi iliyokuwa mahakamani jijini Mombasa.
Kufuatia kesi hiyo, kampuni hiyo ya Uturuki ilitaka pesa hizo za ziada ambazo serikali ya Kenya kupitia Shirika la Huduma za Feri (KFS) imedinda kulipa.
Jana, akizungumza na Taifa Leo, mkurugenzi wa KFS, Bw Bakari Gowa alisema kuwa kikao cha mwisho kimepangwa kati ya serikali na kampuni hiyo ya Uturuki.
“Bado wamesisitiza kulipwa pesa hizo za ziada na ndiposa serikali imeamua kufanya kikao cha mwisho na wao ili kuelewana,” akasema Bw Gowa.
Ziara hiyo ya maafisa wa kampuni hiyo inafanyika wiki mbili baada ya wabunge wa kamati ya uchukuzi kuzuru nchi ya Uturuki kwa ajili ya ukaguzi wa feri hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw David Pkosing, alisema kuwa asilimia 70 ya feri hiyo imekamilika. Hali hiyo, inamaanisha kuwa wakazi wa Mombasa na Kwale wanaotumia kivuko hicho cha Likoni, watalazimika kusubiri kwa muda kabla ya feri hiyo kuletwa.
Bw Pkosing alisema kuwa wanasubiri kuona matokeo ya mkutano kati ya kampuni hiyo na serikali ili kujua feri hiyo italetwa lini.
“Tunashangaa kuona bado kuna mvutano kuhusiana na pesa hizo za ziada. Lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi tunataka kuona pande hizo mbili zinaelewana ili tuweze kupata feri hiyo ili isaidie watu wetu,” akasema Bw Pkosing.
Kamati inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara, itasaidia serikali katika kuendeleza mazungumzo hayo.
Kwa sasa KFS ipo na feri sita ikiwemo ile ya Mv Jambo, Mv Likoni, Mv Harambee, Mv Kwale, Nyayo na Mv Kilindini.
Katika kivuko cha Likoni feri ya Mv Jambo, Mv Nyayo, Mv Kilindini na Mv Harambee ndio zinazohudumu kwa sasa.
Feri ya Mv Kwale inahudumu katika kivuko cha Mtongwe baada ya Mv Likoni kuondolewa kwa ajili ya marekebisho.
Feri hiyo mpya ya Mv Jambo itakuwa feri ya saba na itakuwa na uwezo wa kubeba watu 1600 na magari 64. Feri hiyo pia itakuwepo na vyoo kama ile ya Mv Jambo pamoja na kamera za CCTV.