Mama afariki na mwanawe baada ya kukanyaga waya wa umeme Kwale
FADHILI FREDRICK na DIANA MUTHEU
MAMA na mtoto wake aliyekuwa na umri wa miezi mitatu wamekumbana na kifo baada ya kukanyaga waya wa umeme katika kijiji cha Bowa eneo la Matuga, Kaunti ya Kwale.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Matuga Bwana Joseph Nguli alisema kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 34 na mtoto wake walikuwa wakienda sokoni wakati tukio hilo lilitokea.
“Tuliarifiwa kuhusu tukio hilo na maafisa wetu walikimbilia katika eneo hilo na kuhakikisha kuwa ilikuwa ukweli,” alisema Bw Nguli.
Bw Nguli aliwaomba wakazi wawe na subira kwani kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wamechukua jukumu la kuchunguza suala hilo.
“Hakuna sababu ya kuzua vurugu kwani tukio hili lilitokea kwa bahati mbaya na maafisa wa DCI watachunguza,” alisema.
Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Matuga Isaac Keter alisema kuwa waya huo wa umeme uliokuwa umeanguka haukuwa umerekebishwa kwa karibia wiki mbili sasa.
“Ni huzuni kuwa waya huo umepelekea kupotea kwa maisha ya wakazi wawili wasio na hatia,” alisema, na kuongeza kuwa watajadiliana na Shirika la Kusambaza Umeme Nchini – Kenya Power – kuona jinsi wanavyoweza kuzuia matukio kama haya kutokea tena.
Mwakilishi wa wadi wa eneo hilo, Mwinyi Mwasera aliilaumu kampuni kwa kupuuza wito wa wakazi hao kuwa gogo la nyaya hizo lilikuwa limeoza.
Bw Mwasera alisema alijaribu kuwapigia maafisa simu wiki mbili zilizopita bila mafanikio.
“Tunataka Kenya Power ichukue jukumu kuhusu tukio hilo ambalo limesababisha kupotea kwa maisha ya mama na mtoto wake. Tunataka maafisa hao wahamishwe mara moja,” alisema.
Miili ya marehemu na mwanawe imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti chaHospitali ya Kwale ikisubiri upasuaji.
Kupitia taarifa iliyoandikwa Julai 31, 2020, Kenya Power ilikubali makosa na kusema kuwa watafanya uchunguzi zaidi na kuchukua hatua zitakazohitajika.
“Mtuwie radhi kwa msiba uliotokea eneo la Kombani likihusisha mama na mwanawe. Tutachunguza na kuchukua hatua ifaayo. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia ya wahanga,” ilisema taarifa hiyo.