Habari Mseto

Mamlaka ya KNQA yakagua MKU

September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

MAMLAKA ya Kitaifa ya Kuainisha Kufuzu kwa Asasi za Elimu ya Juu – Kenya National Qualifications Authority (KNQA) – inaendelea kukagua ubora wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kwa lengo la kukipa hadhi ya kuwa kimojawapo cha vyuo vilivyo bora.

Hafla hiyo iliyoendeshwa katika chuo hicho ilihudhuriwa na mkurugenzi mkuu wa KNQA, Dkt Juma Mukhwana, aliyekaribishwa na naibu chansela wa chuo hicho Profesa Stanley Waudo.

Prof Waudo alisema chuo hicho kiko wazi kufanyiwa ukaguzi wa aina yoyote ili kipate mwongozo mwema wa kujiendeleza.

“Chuo chetu kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu inayoambatana na mwongozo uliowekwa na serikali. Kwa hivyo, kwa muda wa siku tano KNQA itakuwa hapa kwa ukaguzi na tuko tayari kufanyiwa ukaguzi wakati wowote ule,” alisema Prof Waudo.

KNQA imepewa uwezo na serikali kuzuru vyuo tofauti nchi mzima kuchunguza hali ya elimu, kutokana na ubora wa masomo, kwa lengo la kuboresha elimu kufikia kiwango cha kimataifa.

Kwa takribani zaidi ya miaka 12 ambayo chuo cha Mount Kenya kimekuwa kwenye ulingo wa masomo, kimetambulika na serikali kwa juhudi zake za kuboresha hali ya elimu.

Baada ya ukaguzi huo chuo hicho kitaorodheshwa na KNQA kuwa miongoni mwa taasisi zinazotambulika nchini.

MKU imejiandaa kwa kufuzu kwa wanafunzi waliokamilisha kazi zao za utafiti. Sherehe hiyo itafanyika kupitia mtandaoni mnamo Oktoba 9, 2020.

Wahitimu zaidi ya 4,000 wanatarajiwa kupokea shahada zao ifikapo wakati huo.

Prof Waudo alithibitisha kuwa kila kitu kipo shwari ambapo chuo hicho kimeweka mikakati jinsi inavyostahili kufanikisha hafla hiyo.