Habari Mseto

Mapasta walimana kwenye mazishi ya mwenzao

September 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

POLISI katika Kaunti ya Kakamega wanawazuilia wahubiri wawili baada ya kupigana katika mazishi ya mhubiri mwenzao na kuzua taharuki iliyotatiza familia ya marehemu.

Wahubiri hao wanadaiwa kuvamiana kwa makonde katika vita vilivyoamuliwa na waombolezaji, baada ya kutofautiana kimaoni kumhusu marehemu, pasta Joseph Musamali.

Inadaiwa kuwa mhubiri aliyepewa jukumu la kuendesha ibada katika kijiji hicho cha Munyuki, eneo bunge la Lugari alikuwa akitumia lugha isiyo ya heshima kwa marehemu na familia yake, jambo ambalo mbali na kuwaudhi waombolezajii lilimkera mhubiri mwenzake aliyekuwa ameketi.

Kulingana na wanawe marehemu, mhubiri huyo alirudia kila mara kuuliza ni vipi familia hiyo ilikuwa masikini sana, na kushangaa ikiwa waliumbwa na Mungu.

“Kabla ya kuondoka kwenda mochari asubuhi, pasta huyo alifika na kuanza kutumia lugha chafu, akiuliza mbona tuko masikini hivi lakini tukatulizwa na kuondoka na majirani zetu,” akasema mwanawe marehemu pasta Musamali.

Lakini waliporejea kutoka hifadhi ya maiti na ibada ya mazishi kuanza, pasta huyo anaripotiwa kuendelea na lugha yake isiyo ya heshima jambo ambalo kadri muda ulivyosonga lilizidi kuwakera waombolezaji.

Anadaiwa kushikilia usemi wake wa kushangaa kwani mwenzake aliyekuwa marehemu alikuwa masikini wa aina gani, ikiwa aliumbwa na Mungu na walikuwa wakiishi vipi dunia hii.

“Sisi tumeshindwa kama alikuja kutufariji ama kutuzomea kuhusiana na hali yetu na ni hapo ambapo walizozana na kuanza kupigana makonde,” akasema mwombolezaji mmoja wa familia hiyo.

Vita vyao vilileta vurugu katika hafla hiyo na kutatiza kuendelea kwake kwa muda, lakini baadaye polisi wakawatia nguvuni mapasta wote wawili ambao ni wa kanisa la PAG.