• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Mapasta washtaki serikali kuzuia ibada

Mapasta washtaki serikali kuzuia ibada

Na MAUREEN KAKAH

MAPASTA watatu wameelekea kortini kutaka agizo la kuondolewa marufuku ya kuendesha ibada, na badala yake hatua ziwekwe kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona makanisani.

Mahakama Kuu jana iliidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamua itajwe Aprili 16.

Jaji James Makau aliidhinisha kesi iliyowasilishwa na mapasta Don Mutugi Majau, Joan Miriti na Alex Gichunge ambao wamewashtaki mawaziri wa Usalama wa Ndani, Afya na Habari na Mawasiliano pamoja na Mwanasheria Mkuu na Inspekta Jenerali wa polisi.

Jaji Makau aliorodhesha kesi hiyo kusikilizwa Alhamisi wiki ijayo na akaagiza mapasta hao kuwakabidhi washtakiwa stakabadhi za kesi kabla ya Aprili 14.

Katika kesi hiyo, mapasta hao wanakubali hatua za serikali za kuzuia kusambaa kwa corona lakini wanasema Wakenya wanahitaji makanisa kutafuta utulivu.

Wanapinga agizo la watu kutokusanyika lililohusisha makanisa kufungwa wakati huu na kwamba uamuzi huo ulifikiwa bila wadau husika kushauriwa.

Mapasta hao wanadai kuwa ibada zinapaswa kuendelea huku wanaohudhuria wakivalia barakoa, glavu na kutumia sabuni zenye dawa.

Wanaendelea kudai kuwa kafyu na agizo la kutokusanyika lilitangazwa na serikali bila kushauriana na makanisa ambayo yangesaidia kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi na kuhubiri amani na umoja huku likitoa misaada ya chakula kwa wasiojiweza.

“Walalamishi pamoja na waumini wengine hawawasilishi kesi hii kortini wakiwa na lengo la kusambaza corona. Lengo lao pekee ni kutaka kukusanyika katika ibada wakifuata masharti yaliyowekwa,” alisema wakili wao John Swaka.

Aliongeza, “Jukumu la makanisa wakati kama wa janga hili linalokumba nchi hii na ulimwengu, ni kuwapa watu matumaini. Kwa unyenyekevu wanaomba mahakama hii kuwasaidia kwa sababu haki na uhuru wao umekiukwa,” alisema.

Walidai kuwa majaji, madaktari na wanahabari wanahatarisha maisha yao wakiwahudumia Wakenya na hivyo basi mapasta pia wanapaswa kuorodheshwa kama wanaotoa huduma muhimu.

Ingawa wanakiri kuwa vitendo vya ibada haviwezi kuendelezwa kama kawaida, walisema mapasta wanatoa huduma muhimu na hawafai kuzuiwa kwa sababu wanafaa kuwa wakisaidia kupiga vita corona kupitia maombi.

Mapasta hao wanataka makanisa waruhuisiwe kuongoza ibada huku viongozi wakihakikisha waumini wamefuata masharti ya serikali.

Serikali ilipiga marufuku ibada makanisani wakati ilipoagiza kusiwe na makongamano aina yoyote kitaifa ili kuzuia ueneaji virusi vya corona.

Tangu wakati huo, makanisa mengi yaligeukia kueneza injili kupitia mitandaoni, televisheni na redioni.

You can share this post!

Habari njema kwa Kenya 22 wakipona coronavirus

Makahaba walilia msaada wakiahidi kubadilika

adminleo