Habari MsetoSiasa

Maraga adai Ikulu ina njama ya kumng’oa mamlakani

November 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

JAJI Mkuu David Maraga amelalamikia kudharauliwa na maafisa serikalini, ambao amedai wanapanga njama katika Afisi ya Rais kuteka usimamizi wa Idara ya Mahakama anayosimamia.

Akizungumza Jumatatu Nairobi kuhusu jinsi Wizara ya Fedha inapunguzia Mahakama bajeti, Jaji Maraga alisema kuna mawaziri na makatibu wa wizara ambao wamefichua kuhusu mipango ya kumng’oa mamlakani kabla mwaka huu uishe.

“Kumbe hii nchi ina wenyewe! Acheni niwaambie, niko hapa kutekeleza wajibu niliopewa na wananchi. Sikuajiriwa na waziri wala katibu wa wizara,” akasema.

Alisisitiza hatajiuzulu ikiwa hilo ndilo lengo la wanaomhujumu bali ataendelea kutetea haki na uhuru wa mahakama.

Kulingana naye, tukio la majuzi zaidi lilitokea Sikukuu ya Mashujaa Dei mjini Mombasa ambapo alikatazwa kutumia njia rasmi iliyotengewa wageni waheshimiwa kufika jukwaani. Pia hakutambuliwa kamwe wakati wageni wakuu walipotajwa.

Kando na hayo, alifichua kwamba wakati anapoitwa kuhudhuria mikutano na hafla nyinginezo Ikuluni, yeye hulazimishwa kusubiri kwa muda mrefu kabla aruhusiwe kuingia huku mawaziri na makatibu wakifululiza na kumwacha mlangoni.

Alidai mawaziri kadhaa wamemdharau kiasi cha kwamba hawawasiliani naye moja kwa moja bali hutumia makarani kumwandikia barua, ambazo alisema yeye huzirarua kwani hawezi kuvumilia kudharauliwa kiasi hicho.

Anaposafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Jaji Mkuu anasema huwa maafisa hawataki atumie chumba cha wageni waheshimiwa wakidai kimetengewa Naibu Rais William Ruto pekee.

Jaji Maraga alipuuzilia mbali ripoti kwamba analalamika kwa kuwa anataka kuishi maisha ya kifahari ikiwemo kuendesha gari aina ya Mercedes Benz, akisema tayari alishanyimwa gari la kifahari na serikali.

“Nimeamua nisipoheshimiwa kama ipasavyo, nitakuwa sihudhurii baadhi ya hafla za kitaifa. Ninaposafiri nje ya nchi huwa napewa taadhima tele. Hapa naambiwa hata chumba cha wageni waheshimiwa siruhusiwi kuingia,” akasema.

Alieleza kuwa, masaibu yanayokumba Mahakama hayakuanza majuzi kwani hata bajeti yao imekuwa ikipunguzwa tangu kipindi cha fedha cha mwaka wa 2013/2014.

Alishangaa kwa nini idara hiyo inaambiwa iwasilishe makadirio yake ya bajeti kwa Wizara ya Fedha ilhali Katiba inahitaji iwasilishwe kwa Bunge la Taifa.

Jaji Maraga alionya kwamba shughuli za mahakama zitaanza kukwama mwezi ujao ikiwa Wizara ya Fedha itaendeleza nia yake ya kuwapunguzia kiasi cha fedha walichohitaji.

Miongoni mwa shughuli zilizo hatarini ni kusikizwa kwa kesi za ufisadi, kesi za rufaa, mahakama tamba ambayo huzunguka maeneo ya mashinani.

Kufikia Julai 2018, Mahakama ilikuwa imeomba jumla ya Sh31.2 bilioni katika kipindi hicho cha fedha lakini Wizara ya Fedha ikatoa Sh17.3 bilioni pekee.