Maraga kukamilisha kipindi chake leo Ijumaa
Na RICHARD MUNGUTI
JAJI Mkuu David Maraga atang’atuka ofisini leo Ijumaa baada ya kuhudumia Idara ya Mahakama kwa miaka minne katika wadhifa huo baada ya kutimiza umri wa miaka 70 ambao ndio umri wa majaji kustaafu.
Jaji Maraga aliyetwaa hatamu za uongozi wa mahakama mnamo Oktoba 2016 kutoka kwa Dkt Willy Mutunga, atakumbukwa kwa kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta ya 2017.
Katika kipindi chake, Jaji Maraga aliheshimiwa kwa ukakamavu katika kutetea uhuru wa Mahakama.
Kuondoka kwa Jaji Maraga kutatoa fursa kwa naibu wake Jaji Philomena Mbete Mwilu kutekeleza majukumu yake kabla ya Tume ya Mahakama (JSC) kuanzisha mchakato wa kumsaka mridhi wake.
Lakini Jaji Mwilu tayari ameanza kupata viunzi katika utekelezaji kazi ya Jaji Mkuu baada ya mwanaharakati Okiya Omtatah kuwasilisha kesi katika Mahakama kuu.
DPP na DCI waliwasilisha kesi mbili katika JSC wakiomba Jaji Mwilu atimuliwe kazini kwa utovu wa kimaadili.
Jaji Maraga alitangaza kung’atuka kwake mamlakani Desemba 7,2020 akiwa katika Mahakama ya Manga katika Kaunti ya Nyamira alipoifungua rasmi.
Alisema, “Ijumaa (Desemba 11, 2020) ndiyo itakayokuwa siku yangu ya mwisho kuhudumu katika wadhifa wa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Kenya.”
Alisema ataanza likizo itakayotangulia kustaafu kwake rasmi Januari 2021.